NEC yatangaza uchaguzi Mbarali, kata sita

 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Mbarali, mkoani Mbeya na kata sita za Tanzania Bara utafanyika Septemba 19, 2023.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima akitangaza uchaguzi huo leo Jumamosi, Agosti 5, 2023 amesema wagombea watachukua fomu kuanzia Agosti 13-19, 2023.

Amesema uteuzi utakuwa Agosti 19, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Agosti 20, 2023 hadi Septemba 19, 2023.


Amezitaja kata zitakazofanya uchaguzi mdogo ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.

“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,” amesema Kailima.

Amesema NEC imetoa taarifa hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Tanzania, akiitaarifu Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Mbarali.

Jimbo hilo limekuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Mbarali (CCM), Francis Mtega, kufariki dunia Julai 1, 2023 kwa ajali ya kugongwa na trekta (Power Tiller) shambani kwake Mbarali, mkoani Mbeya.

“Tume imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa, akiitarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara. Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,” amesema Kailima.


Ameongeza, “Tume kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Mbarali na Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara.”

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments