Rais Samia apiga marufuku kuingilia utendaji mashirika ya umma

 Rais Samia Suluhu Hassan, amepiga marufuku mawaziri na watendaji wa Serikali kuingilia utendaji wa mashirika ya umma nchini kwa maslahi yao binafsi.

Rais ametoa onyo hilo leo jijini hapa, wakati akifungua kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, mkutano ambao unaowajuisha pia wajumbe wa bodi, mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine.

Rais Samia ametaka taasisi na mashirika hayo yaachwe yajiendeshe bila wizara kutia mikono.


Tanzania in taasisi na mashirika ya umma 248, ambazo kwazo, Serikali imewekeza Sh73 trilioni, hata hivyo, bado mchango taasisi na mashirika hayo kwenye pato la Taifa, huku kuingiliwa katika utendaji kukitajwa kuwa moja ya changamoto.

Hata hivyo, amesema watendaji wa mashirika hayo, wanatakiwa kubadilika kifikra na hivyo kufanya kazi kwa weledi na hatimaye kuongeza mapato na tija kwa taifa, badala ya mashirika hayo kuendelea kuwa tegemezi kwa Serikali.

Amesema sasa watendaji wa mashirika ambao watashindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha hasara watafikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa upande mwingine Rais Samia amebainisha juu ya baadhi ya taasisi na mashirka ya umma nchini, ambayo yamekuwa sehemu ya watu kula raha wakati hayaonekani kuwa na tija kwa Serikali.

“Mashirika yamekuwa ni sehemu ya kula raha, na ndio maana tulivyokuwa tunazungumza, Waziri wa Utumishi akasema; tunapozungumza mashirika haya, pale kwangu utumishi nina vita," amesema na kuongeza;

"Kila mtu anataka kuhama Serikalini kwenda kwenye mashirika, kuna nini? Marupurupu mazuri mishahara minene lakini hakuna tija kwa serikali, sasa hatuwezi kwenda hivyo ndugu zangu, lazima tubadilike.”

Hivyo Rais Samia amezitaka taasisi na mashirika hayo kuondoa visababishi vya kutofanya vizuri ili Serikali iongeze mtaji, ambao utasaidia kuzifanya ziwe na tija.


“Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanya uchambuzi na kubaini taasisi ambazo majukumu yake yanashabihiana, wengine majukumu yao hayana maana tena sasa hivi," amesema na kuongeza;

"...lakini kuna taasisi ambazo utendaji kazi wake unalegalega mno, na sababu zake zimejulikana, sasa tuziondoshe ili tuweke mtaji na waweze kufanya kazi. Tunafanya hivyo kwa sababu takwimu zinatuonyesha kwamba asilimia 17 ya ajira ndani ya nchi inatolewa na mashirika na taasisi za umma, kwahiyo hatuwezi kuyaondoa."


Rais Samia amesema Serikali yake haiwezi kuruhusu ajira hiyo kupotea, na amewahakikishia watendaji hao kuwa katika maboresho ambayo yanafanyika, hakutakuwa na nguvu kazi au ajira yeyote itakayopotea.

"Wote wapo kwenye mashirika, aidha watapelekwa kwengine au yatakuja mashirika mengine ambayo yana maana zaidi sasa hivi, kuliko wakati yalipoanzishwa na hakuna ajira itakayopotea.” amewahikikishia.

Hata hivyo amewata watendaji ambao hawawezi kuendeana na maboresho hayo, kumfuata na kumnong’oneza ili awabadilishie kazi kuliko kusubiri yeye awapangue.

Akizungumzia maboresho ya Mashirika ya Umma, amesema kuna mashirika yataunganishwa na mengine kuondolewa.

Hata hivyo ameagiza Ofisi ya hazina, kuzungumza na mashirika hayo na kupata maoni yao kabla ya kuunganishwa ama kufutwa.

"Nendeni mkawasikilize kabla ya kutoa maamuzi, kama wakiwashawishi kuwa wanaweza kuboresha utendaji kazi wao basi watazamwe," amesema.

Katika namna ya kutambua na kuthamini mchango wa mashirika hayo katika utendaji kazi, Rais amekabidhi tuzo kwa baadhi ya mashirika hayo kwa kuwa yamefanya vizuri, ikiwepo kutoa gawio kubwa kwa Serikali.


Akiyataja mashirika hayo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, taasisi hizo kimsingi zimetoa mchango mkubwa kwa taifa.

Huku akitaja Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambao wamechangia kiasi cha Sh272.4 bilioni, huku Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ikishika nafasi ya pili kwa kuchangia Sh207.9 bilioni.

Kwa mujibu wa Msechu, taasisi ya tatu kwa kufanya vizuri ni Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Kwa upande wa mashirika ambayo Serikali ina hisa na yanafanya vizuri, Twiga Cement imeshika namba moja kwa kuchangia Sh84 bilioni, ikifuatiwa na Benki ya NMB, ambayo imechangia Sh45 bilioni huku ya tatu ikiwa ni kampuni simu ya Airtel, ambayo ambayo imechangia Sh61 bilioni.

Taasisi zingine zilizopewa tuzo kwa kufanya vizuri ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Bima la Taifa (NIC), ambapo STAMICO iliyokuwa hatarini kufutwa miaka miwili iliyopia, mwaka huu wamechangia Sh2.2 bilioni huku NIC nayo ikifanya maboresho makubwa ya kuitendaji na kupata faida ya Sh2 bilioni.

Rais pia ametoa tuzo kwa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), ambalo lilipata faida ya Sh240 bilioni.

Mashirika mengine yaliyopewa tuzo kwa kuchangia gawia kwa Serikali pamoja na Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC), lilichangia Sh2.5 bilioni.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kumekuwepo na maboresho katika utendaji kazi kwa baadhi ya mashirika, hata hivyo, bado kuna changamoto.

"Wito kwa watendaji wote wamashirika ya umma ni muhimu kuyazingatia yote ambayo Rais Samia Suluhu ataagiza ili kutoa msingi wa mwelekeo mpya wa Mashirika ya umma" amesema.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments