Rais Samia aridhia mapendekezo ya ‘kufumua’ mashirika

 

ARUSHA: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema ameridhia mapendekezo ya kufanya mageuzi makubwa katika Mashirika na Taasisi za Umma ili kuongeza ufanisi na kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa.

Pia amesema Serikali inatunga sheria kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Mamalaka. Rais Samia amesema leo Jijini Arusha wakati wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho cha siku tatu, Rais Samia amesema amepokea mapendekezo ya kufanya mabadiliko makubwa katika taasisi za umma ambazo kiutendaji zinasimamiwa na ofisi hiyo.

“Nimeridhia mapendekezo hayo,” amesema Rais Samia. Hata hivyo ameiomba Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya Msajili wa Hazina kukutana na wadau kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mapendekezo hayo.

Mapendekezo yaliyoidhinishwa na Rais Samia ni pamoja na kufuta baadhi ya mashirika, kuunganisha baadhi ya mashirika na kuanzisha mashirika mapya.

Bado haijawa wazi ni mashirika gani yamefutwa ama kuunganishwa, lakini Rais Samia ametaka kuwe na mazungumzo upya na wadau kubaini iwapo kuna sababu zingine za kutotekeleza mapendekezo mapya.

Kwa mujibu wa Rais Samia mabadiliko yanayopendekezwa hayalengi kufuta ajira bali kuboresha utendaji kazi wa mashirika ya umma. Amesema: “Tunataka kupunguza mzigo kwa serikali.”

Wakati huo huo Ofisi ya Msajili wa Hazina imezitambua taasisi na mashirika yaliyofanya vizuri katika mwaka wa fedha 2022/23. Taasisi hizo ni pamoja na Mashirika ya Umma yaliyotoa gawio kubwa zaidi ambapo Taasisi hizo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Vilevile, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilizitambua Kampuni za Twiga Cement, Benki ya NMB na Airtel Tanzania kama Taasisi binafsi ambazo serikali inahisa. Rais Samia pia alitoa tuzo kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Bima la NIC Insurance kama makampuni yaliyofanya mapinduzi kutoka kuwa orodha ya mashirika yaliyokuwa hatalini kufutwa hadi mashirika yanayochangia gawio.

Taasisi zilizotambuliwa kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiutendaji ni pamoja na Shirika la Ugavi – Tanesco na NIC Insurance. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments