Recent-Post

Serikali yachanja mbuga, uwekezaji bandari

Serikali imesema inaandaa nyaraka kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano ya uwekezaji wa bandari kati yake na Dubai.

Hatua hiyo inakuja wakati bado kukiwa na ukinzani wa maoni, kuhusu makubaliano hayo kutoka kwa makundi mbalimbali nchini.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano Jumamosi Agosti 26, 2023, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alieleza hatua hiyo inafuata baada ya Serikali kushinda kesi hivi karibuni.


“Hakuna ukimya, Serikali ilishasema kwamba inapokea maoni ya Watanzania, baada ya kukamilisha michakato yote. Bunge limeridhia, hatua inayofuata sasa ni kuandaa nyaraka. Zikikamilika ndiyo tunakwenda kuandaa miradi ya utekelezaji,” alisema Msigwa alipojibu swali la John Marwa wa Jambo TV.

“Kinachofanyika ni hivi; baada ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai ni mikataba ya utekelezaji. Hii mikataba ndiyo itakayosema sasa mradi wetu utakuwa namna gani, tunashirikiana kwenye eneo gani na mikataba hii itakuwa mingi, hautakuwa mmoja.

“Kama ni mkataba wa mifumo bandarini, ushushaji na upakuaji wa mizigo; kama ni mikataba ya kujenga maeneo ya kuhifadhi, kwa kadiri tutakavyokubaliana tutakuja kuwajulisha,” aliongeza Msigwa.

Upokeaji maoni unaendele

Hata hivyo, alisema bado wanasikiliza maoni ya wananchi kupitia njia mbalimbali.

“Kwa hiyo wadau wakizungumza, Serikali tunapokea hayo maoni tunazingatia na wawekezaji tutakaoshirikiana nao. Majadiliano ni pamoja na kupokea maoni,” alisema Msigwa, huku akisisitiza kuwa bandari haijauzwa.

“Mpaka sasa hakuna mradi wowote wa utekelezaji tuliosaini, tulichosaini ni makubaliano ya ushirikiano ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwamba tutashirikiana kwenye uendelezaji wa bandari. Tunaendeleza wapi, kwa kiasi gani, kwa muda gani, itakuwamo kwenye mradi.”


Akifafanua kuhusu njia za kupokea maoni, Msigwa alisema kama Bunge lilivyopokea maoni ya wananchi na kuridhia makubaliano hayo, Serikali pia, inaendelea kuyapokea kupitia ofisi za wakuu wa mikoa, wizara na mikutano ya hadhara.

Makubaliano hayo yaliyotiwa saini na Serikali Oktoba 25, 2022 yaliibua gumzo na yaliridhiwa na Bunge Juni 10, 2023.

Maoni kinzani

Julai 9 mwaka huu, Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyajadili na kuelekeza viongozi wa chama hicho na Serikali kutoka kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusu mkataba huo.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na viongozi wa Serikali, akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa, Kitila Mkumbo walizunguka mikoani na kufanya mikutano ya hadhara kutekeleza agizo hilo.

Kwa upande wake, Chadema imeanzisha operesheni wanayoita, ‘+255 Katiba Mpya- Okoa bandari zetu,’ ikipinga mkataba huo.

Makundi ya wasomi, viongozi wa dini, wanasheria na wanasiasa wamekuwa wakivutana kuhusu makubaliano hayo.

Miongoni mwa wasomi waliokosoa makubaliano hayo ni gwiji wa sheria, Profesa Issa Shivji, Dk Rugemeleza Nshala, Waziri wa zamani Profesa Anna Tibaijuka na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Agosti 18 mwaka huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) lilitoa waraka unaokosoa makubaliano ambao waumini walisomewa makanisani wakati wa misa.

Akizungumza Agosti 21, katika maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), yaliyofanyika mkoani Arusha, Mkuu wa kanisa hilo, Dk Fredrick Shoo aliyemaliza muda wake alibainisha kuwa kanisa hilo linaunga mkono uwekezaji.


“Hatupingi uwekezaji Mheshimiwa Rais na tunajua wewe katika nia yako unataka wawekezaji. Hata hivyo, jambo hili limekuwa na maoni mbalimbali ya wananchi na vyombo vya habari, viongozi wa dini zote na kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Askofu Shoo.

Jana Ushirika wa Wachungaji wa Kipentekoste nchini (PPFT), ulimuomba Rais Samia kufunga mjadala wa mkataba huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkuu wa Kanisa la Matendo Makuu Tanzania na mwenyekiti wa PPFT, Askofu Pius Ikongo, alizungumzia ukimya wa Rais akisema una faida, ila kuendelea kunyamaza zaidi, kunaweza kuleta madhara.

Basuta yaonya

Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Jumuiya za Ansaar Sunna (Basuta) lilieleza kuwa Tanzania ni kubwa, hivyo baadhi ya watu wasijitwishe ukiranja wa kuwasemea wengine ilhali wako hai na wana haki za kiraia kama walizonazo wao.

Katibu Mkuu wa Basuta, Sheikh Shaaban Musa kupitia waraka uliotolewa wiki hii, alisema katika mjadala hawaridhishwi na undumilakuwili na ukosefu wa uadilifu wa wapingaji wa mkataba waliofumbia macho mikataba mingi na ya ovyo zaidi huko nyuma.

“Basuta tusingependa kujikita kwenye mjadala wa vipengele mahususi wa mkataba wenyewe, tukiamini mchakato unaenda vizuri na maslahi mapana ya Taifa yatafikiwa, ‘‘ ilisema taarifa ya Basuta.

Awali, vijana wanne kutoka mikoa tofauti, wakiwamo wanasheria watatu, walifungua kesi ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, wakipinga makubaliano hayo ya uwekezaji wa bandari.

Hata hivyo, Agosti 10 mwaka huu, Mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo ikielekeza kuwa hoja za walalamikaji hazina mashiko.


Marekebisho ya sheria

Kwa upande mwingine, Msigwa alifafanua hatua ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, kusitisha kupokea maoni kuhusu maboresho ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu umiliki wa rasilimali asilia, akisema: “Bunge ni mhimili mwingine, tunaendelea kufanya mawasiliano. Serikali inakwenda kujibu. Inawezekana jibu lilikosekana siku ile, lakini litapatikana siku nyingine.”

Juzi, kamati ilisema imeshindwa kupokea maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu na umiliki wa mali na rasilimali asilia na ile ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya mali na rasilimali asilia, kwa sababu kuna hoja ambazo Serikali imeombwa kuzitolea ufafanuzi.

Sheria hizo mbili ni kati ya tano zilizomo katika muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba 2 wa mwaka 2023.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Joseph Mhagama alisema hoja wanazoomba wapatiwe ufafanuzi na Serikali ili waweze kujiridhisha wakati wa uchambuzi wa marekebisho hayo, zinahusiana na maudhui ya mabadiliko ya sheria hizo.

Nyongeza na Fortune Francis na Janeth Mushi.

Post a Comment

0 Comments