Shirika la Madini la Taifa labadili ‘upepo’, latunukiwa tuzo

Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limesema wanalifanyia kazi agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuyataka mashirika ya umma kuwekeza nje ya nchi, limewapa chachu ya kuwaza zaidi ili kuisaidia Serikali kutatua changamoto mbalimbali kutokana na mapato yatakayopatikana.

Rais Samia alitoa agizo hilo jana Jumamosi, Agosti 20, 2023 jijini Arusha alipofungua kikao kazi cha wakurugenzi na wenyeviti wa bodi wa taasisi na mamlaka za Serikali kinachomalizika kesho Jumatatu, Agosti 21,2023.

Rais Samia alisema kama ambavyo kampuni za nje zinawekeza nchini na faida kurudisha kwao na kutoa wito kwa mashirika ya ndani kufanya hivyo kama ambavyo Benki ya CRDB imefanya hivyo.

Katika hafla hiyo, Rais Samia alikabidhi tuzo kwa taasisi na mashirika mbalimbali ikiwemo Stamico lililoibuka mshindi wa kwanza katika taasisi za umma zilizofanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji na yenye tija kwa mwaka 2023.

Ni baada ya kufanyika kwa mabadiliko ndani ya shirika hilo, lilinyakua tuzo ya pili katika kundi la mashirika ya umma ambayo yametoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, Dk Venance Mwasse alisema,“kwa hiyo hilo tumelichukua, tunakwenda kuliweka kwenye mikakati yetu kwamba miradi ya shirika sio lazima iwe hapa Tanzania lakini lazima tufikiri kwenda kuwekeza kwenye nchi zingine na kuleta kipato nyumba kitakachoisaidia serikali kutekeleza majukumu yake na hayo ndio majukumu hasa ya mashirika ya umma.”

Tuzo hizo zilikabidhiwa juzi jijini Arusha na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyefungua kikao kazi hicho na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk. Venance Mwasse pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya STAMICO, Meja Jenerali (Mstaafu) Michael Isamuhyo. 

Dk Mwasse mbali na kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufikia mafanikio hayo, alisema tuzo hizo zimewapa furaha na kuthibitisha ukiamua na kutenda jambo inalipa.

Alisema kabla ya kufikia mafanikio hayo, kwanza walimuelewa Rais Samia kwamba anataka nini hasa ikizingatiwa anataka tija kwa mashirika ya umma.

 "Kwa hiyo menejimenti, bodi na watumishi wote tumekuwa tunatekeleza hayo kwa kufanya maamuzi sahihi ambayo yanalenga kuleta tija kwa jamii ndio maana tumeona
STAMICO limetoka kwenye orodha ya kufutwa na kuwa shirika la mfano," alisema. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alisema Serikali inatambua zipo taasisi na mashirika ya umma yanayofanya vizuri na kujipambanua katika makundi yanayotoa gawio kwenye mfuko wa serikali, kuongeza uzalishaji wenye faida na kufanikiwa kujitegemea. 

"Tumeambiwa mashirika haya ndio nguzo kuu ya maendeleo ya Serikali, nguzo ya uchumi wa serikali. Yakizalisha wa vizuri Serikali inapata tija na kufanya makubwa zaidi, yakiwa mzigo inarudisha nyuma maendeleo ya serikali," amesema Rais Samia. 

Awali, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliipongeza Stamico na kubainisha katika miaka miwili iliyopita ilikuwa inafikiriwa kufutwa kutokana na utegemezi lakini sasa wameweza kuchangia hadi gawio kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

Kauli hiyo pia iliwahi kuungwa mkono na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko hivi karibuni ambaye aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Stamico kwa kulifufua shirika hilo ambalo awali lilikuwa hoi lakini sasa limeongeza tija na hata kushinda zabuni ya kuchoronga miamba ya madini ya kampuni kubwa duniani ikiwamo Anglo Gold Ashanti kupitia kampuni yake ya Geita Gold Mining Limited (GGML).


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments