VIONGOZI wa vyama vya siasa wamekemea vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaotumia vibaya nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kutoa lugha za matusi, udahalilishaji na kuugawa muungano.
Wakizungumza katika mKutano wa vyama vya siasa ulioandaliwa na baraza la vyama vya siasa nchini jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof Ibrahim Lipumba amesema katika kufanya mikutano mwanasiasa anaweza kuwa na hoja zake za bandari na akaziwasilisha bila kutaja habari za muungano.
“Ni muhimu mambo haya tukatazama tutumie busara kufanya mikutano mnataka kurudi tunakotoka? yule Bwana alikuwa akiongea wote kimya sasa mnahitaji turudi huko?ameuliza.
Amewataka wanasiasa kutumia nafasi hiyo vizuri na pia kumsubiri Rais Samia aweze kutekeleza yale aliyoyaahidi na kukosoa kistaarabu.
Mwenyekiti wa Chama Cha United Democratic Part (UDP) John Cheyo amesema tangu kufunguliwa kwa mikutano ya kisiasa kidogo kuna mambo yanatia wasiwasi kwani kuna mengi ambayo hawajawahi kuona na wanayaona sasa ambayo yanazungumzwa wazi wazi kama kuvunja muungano hali inayoleta simanzi.
“Sasa tunasikia matusi hadi kiasi cha kudhalilisha kiongozi wa nchi na sasa wanaweza kwenda mataifa mengine kushambulia nchi yao uzalendo uko wapi?tunajiuliza tukiendelea hivi tutakuwa na umoja na tutaendelea kuwa na amani tukaona kwanini tusiite kikao cha wadau tuzungumze,”ameeleza Cheyo.
0 Comments