Vituo 17 vya utafiti kuboreshwa miundombinu

 

VITUO 17 vya Utafiti wa Kilimo Tanzania vitawekwa miundombinu ya umwagiliaji, ili viweze kufanya shughuli zake za kiutafiti pamoja na upandaji wa mbegu kwa mwaka mzima.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk Geofrey Mkamilo amesema hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu mikakati ya serikali ya kuboresha kilimo nchini.

Dk Mkamilo amesema kupitia Wizara ya Kilimo zimetengwa sh bilioni nane kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika vituo 17 vya TARI vilivyopo nchi nzima.

Amesema fedha hizo zitatumika kujenga miundombinu hiyo katika hekta 854, ambako ni kwenye vituo vyote 17 vya utafiti nchini.

Amesema mpaka sasa ujenzi huo umeanza kwa maana ya kwamba ameshapatikana mkandarasi anayejulikana kama Pro Agro Global Limited na mikataba imeshasainiwa mwaka wa fedha uliopita.

“Mkandarasi huyu ameshatengeneza ramani, kuna sehemu anachimba mabwawa na kujenga matenki ya maji. Kazi ya usanifu imeshaanza kwenye vituo vyote. Mwaka huu wa fedha ulioanza Julai kuna bajetii y ash bilioni nane kwa ajili ya kuendelea na ujenzi,” amesema.

Amesema kama jukumu la taasisi hiyo lilivyo la kutafiti, kusimamia, kuhamasisha na kuratibu shughuli za utafiti nchini, kupitia miundombinu hiyo ya umwagiliaji itaongeza tija katika kilimo.

Pia miundombinu hiyo itasaidia uzalishaji wa mbegu kwa mwaka mzima, badala ya kuzalishwa mbegu kipindi kifupi zitaendelea kuzalishwa mwaka mzima.

Ametaja vituo vinavyojengwa miundombinu hiyo ya umwagiliaji kuwa ni TARI Maruku kilichoko Bukoba, Ukiliguru Mwanza, Tumbi Tabora, Kihinga Kigoma na Uyole Mbeya.

Vituo vingine ni Kifyulilo Iringa, Naliendele Mtwara, Kibaha Pwani, Mikocheni Dar es Salaam, Dakawa Mvomero, Ifakara Kilombero, Ilonga Morogoro na Hombolo Dodoma.

Vingine ni Makutupora Dodoma, Mlingano Tanga, Tengeru Arusha na Selian Arusha.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments