Watumishi 7 halmashauri kizimbani uhujumu uchumi

KATAVI; Mpanda. TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, watumishi 7 kwa tuhuma za wizi wa fedha kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 1. 23.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5 ya mwaka 2023, imetajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Gway Sumaye na mwendesha mashtaka Gregory Mhangwa, ambapo amesema watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa makosa matatu ya kujihusisha na genge la uhalifu, uhujumu uchumi na wizi.

Mhangwa ameeleza kuwa washitakiwa hao walishirikiana kutenda makosa hayo kati ya Novemba 1, 2022 hadi Agosti 11, 2023 huko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kwa kudanganya kuwa walikuwa wakiwalipa wakandarasi waliofanya kazi katika Halmashauri hiyo kiasi cha Sh 1,232,408,689 na kuisababishia hasara halmashauri.

Waliopandishwa kizimbani ni Canuthe Matsindiko (41), ambaye ni Ofisa TEHAMA kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Michael Katanga (31), Mhasibu wa Halmashauri ya Mpimbwe, Tamaini Misese (47), aliyekuwa Ofisa TEHAMA Mkoa wa Katavi na Maira Samson Olumba (38), Ofisa Manunuzi wa Halmashauri ya Mpimbwe.

Wengine ni Emmanuel Damas Saranga (37) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe, Masami Andrew Mashauri (49) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe na Laurent William Sunga (33) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe.

Washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi Septemba 4, 2023 kesi hiyo itakapotajwa tena katika Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga.
Chanzo Habari leo

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments