Zifahamu athari za ulaji vyakula safarini

Je, ni tabia gani za wasafiri imewahi kukukera wakati wa safari kutoka eneo moja kwenda lingine? Yapo mambo manne yanayotajwa kutokea safarini ambayo yanakera na yanaweza kuhatarisha afya ya mlaji.

Inawezekana ni namna abiria mwenzako anavyochanganya vyakula au uongeaji wake mwanzo hadi mwisho wa safari, kuongea na simu kwa sauti ya juu au kula chakula kisicho salama na bila mpangilio na hivyo kusababisha kero kwake na kwa wenzake.

Inapotokea ukala chakula kisicho salama huwa na athari mbalimbali kiafya kama kuumwa tumbo, kutapika, kuhara, kuhara damu na mengine ya muda mrefu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha watu milioni 600 duniani (mtu mmoja kati ya 10), huugua kila mwaka kwa kula chakula kisicho salama na kati yao, 420,000 hufariki dunia, 125,000 wakiwa watoto chini ya miaka mitano.

Licha ya takwimu hizo za jumla, usalama wa vyakula safarini ni changamoto, kama anavyosimulia Sarafina Kileo, mkazi wa Siha mkoani Kilimanjaro kuhusu safari yake ilivyokuwa ngumu, baada ya kuuziwa chakula kisicho salama

Akizungumza na gazeti hili, anasema akitokea Mbeya Mbeya kwenda Dar es Salaam walisimama kwa ajili ya chakula lakini ubora wa chakula hicho haukuwa wa kuridhisha.

“Tofauti na mimi niliyeumwa tumbo, wengine walitapika. Hakikuwa salama kwa kuwa kilikaa muda ndipo kikapashwa,” anasema.

“Jambo ambalo mimi nililiona pia ni hatari ni kunywa soda na korosho au kula korosho na mayai ukiwa safarini, lazima utapitia changamoto ya kiafya,” anaeleza.

Ushuhuda wake mwingine, unahusu kwa mtu aliyemuona kwenye basi akinywa mtindi na baadaye akapata kichefuchefu na akatapika.

Kisa hicho hakina tofauti sana na cha Hamis Ibrahim, mkazi wa Arusha, aliyesema wakati akitokea Dar es Salaam kwenda Arusha waliuziwa chakula kilichoharibika kwenye moja ya hoteli.

“Tulifika kwenye hiyo hoteli tukaambiwa dakika 10 kula, hakuna abiria aliyeweza kula pale sote tulichukuwa vyakula ambavyo tayari vilifungwa,” anasema.

“Mimi nilihitaji chipsi na kuku, nilibeba nikale kwenye gari, nilipofungua nikakuta hazijatengenzwa siku hiyo na kuku alimpakwa unga wa ngano na hakuwa ameiva,” alieleza.

Kwa mujibu wa Ibrahim, aliyekuwa na njaa, alikula hivyohivyo na baada ya muda alianza kupata maumivu ya tumbo na kumlazimu kutumia dawa.

Ibrahim anasema, kutokana na kadhia hiyo tangia ya hapo anaposafiri hulazimika hubeba chakula kutoka nyumbani.

Kula holela

Ipo pia sikumuliza ya Juliana Fredy, mkazi wa Mbezi jijini Dar es salaam. “Nilikuwa natokea Mwanza kwenda Dar es Salaam kwa basi, abiria mwenzangu alinunua parachichi bila kuliosha akala. Mbele kidogo akanunua tena mahindi akala, yaani kila kitu kilichokuwa kinauzwa eneo ambalo basi lilisimama alinunua na kula,” anasimulia Fredy.

Alisema baada ya muda, jirani huyo alianza kusikia tumbo la kuharisha akaomba dereva alisimamishe basi akajisaidie vichakani.

Hali hiyo iliwasumbua abiria wengi njiani hatua ambayo ilisababisha abiria wenzake kumrushia maneno yasiyo na staha kutokana na aina ya ulaji wake.

Mpaka safari imekamilika, Juliana anasema jirani yake huyo alisimamisha gari mara mbili kutokana na tatizo la tumbo.

Simulizi nyingine ni ya Msafiri Juma aliyekuwa akisafiri kutoka Kigoma kwenda Dodoma. Anasema wakiwa njiani aliingia mtu akiuza nyama ya kukaanga, ya kuchoma, ndizi na chips na kiuhalisia havikuwa vya moto na hivyo kuwa hatarishi.

Hatua zinazochukuliwa

Ili kudhibiti uuzwaji wa vyakula vilivyoharibika wakati wa safari, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Yusuph Ngenya anasema ni muhimu kila abiria anayepitia changamoto hiyo wakati wa safari atoe taarifa TBS.

“Kama abiria atajua ametumia chakula eneo fulani na akapata madhara awasiliane nasisi tuchukue hatua za haraka,” anasema Dk Ngenya.

Kauli kama ya TBS inatolewa pia na Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo kuwa endapo abiria wanauziwa vyakula vilivyoharibika wanapaswa kutoa taarifa haraka kwa madereva wao ili hatua zichukuliwe.

“Hiyo ni biashara kama itabainika abiria akitoa taarifa huyo aliyefanya kitendo hicho kaua biashara yake kwa kuwa taarifa tutazisambaza kwa haraka. Sisi kwenye hoteli tunazosimama tunazingatia ubora, kama kuna changamoto abiria watoe taarifa wasibaki nazo,” alisema.

Vyakula hatari wakati wa safari

Ofisa Afya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ally Babu anasema usafi wa chakula hutegemea usafi wa mwandaaji, mazingira na malighafi yaliyotumika.

Babu alisema kama chakula kimeandaliwa katika mazingira ambayo si salama ni rahisi kuingiliwa na bakteria, sumu au vitu vingine kama mchanga na vumbi.

Wakati wa safari, anasema vyakula vyenye protini hasa nyama, ya kuku, ng’ombe, samaki, maziwa na mazao yake visipofuata kanuni bora za utayarishaji na uhifadhi kuna hatari ya kuingiwa na uchafu. “Hata juisi inayotengezwa kwa matunda kama imetayarishwa katika mazingira machafu kuna hatari ya kusababisha madhara kwa mnywaji,” anasema.

Babu anasema hatari ya ulaji safarini huanza pale mwandaaji au muuzaji anaposhika bidhaa zake na mikono michafu.

Alitolea mfano, mtu anaweza kuuza bidhaa hizo barabarani na wakati mwingine kwenda haja kubwa au ndogo pasipo kusafisha mikono vizuri hali ambayo huingiza uchafu katika vyakula jambo ambalo kwa mlaji ni hatari.

Babu anasema hata muda mfupi wanaopewa abiria kwenda kuchukua chakula na kuchimba dawa wakati wa safari huongeza hatari ya watu kula chakula kichafu.

“Chakula pia kinaweza kutayarishwa salama lakini mlaji akakichafua,” alisema Babu.

Kinachopaswa kuzingatiwaBabu anasema muandaaji wa chakula anapaswa kuwa msafi na asiye na magonjwa ya kuambukiza.

“Hatari ya mtu mwenye magonjwa ya kuambukiza kuandaa chakula cha abiria na watu wengine ni kutengeneza uwezeakano mkubwa wa kuwaambukiza watu wengine maradhi yake,” alisema.

Mathalan, Babu anafichua kwamba wapo watayarishaji wa chakula huchokonoa pua kwa vidole na kuendelea kushika chakula anachokiandaa.

“Mtu anatumia nguo yake kusafisha chombo au kushusha jikoni hiyo pia ni hatari, kama nguo yake itakuwa na vimelea, atakuwa anakichafua pia chakula,” alisema.

Kwa mujibu wa Babu, uchanganyaji wa chakula, hufanya mmeng’enyo wake kutofanyika vizuri na kusababisha tumbo kujaa gesi inayofanya mtu achafukwe na tumbo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments