KILIO CHANGAMOTO SOKO LA MAHINDI LUDEWA CHAIFIKIA KAMATI YA SIASA MKOA WA NJOMBE

Kutokana na Wakala wa Taifa  wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kusitisha zoezi la ununuzi wa mahindi kwa wakulima wilayani Ludewa mkoani Njombe kwa takribani wiki tatu sasa wakulima hao wameiomba serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendeleza zoezi la ununuzi huo.


Wakulima hao wamewasilisha ombi hilo mbele ya kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi mkoani Njombe walipofanya ziara katika kata 18 kati ya 26 za wilayani humo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho katika miradi mbalimbali ambapo imeongozana na viongozi wa CCM wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na wakuu wa Idara mbalimbali ngazi ya wilaya na Mkoa.

Antony Haule ni miongoni mwa wakulima hao amesema kuwa wakati NFRA wakinunua mahindi hayo iliwasaidia kuwaepusha na walanguzi waliokuwa wanapita mitaani kununua mahindi hayo kwa gharama ndogo lakini wanaishukuru serikali kuwaongezea bei ya ununuzi kutoka bei ya awali ya sh. 400 hadi 500 kwa kilo na kufikia sh. 860 hadi sh. 900 kitu ambacho kilileta hamasa kwa wakulima hao kupeleka mahindi yao kwaajili ya kuyauza NFRA lakini toka zoezi lisitishwe wamejikuta wakibakiwa na mahindi mengi nyumbani na kuishia kuyauza tena kwa walanguzi.

"Mahindi ambayo yamenunuliwa ni machache sana ukilinganisha na tuliyo bakinayo majumbani kwetu, tunaomba serikali iturejeshee ile furaha waliyotuanzishia ili nasi wakulima tuweze kunufaika na kilimo chetu na kukiona chenye tija kwani endapo tutauza tena kwa serikali itatuwezesha kupata mitaji mizuri kwa ajili ya kilimo cha mwaka huu". Amesema Haule.

Aidha kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa wa Njombe Julius Peter amesema serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mwenyekiti wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kwaajili ya kutatua kero mbalimbali za wananchi hivyo changamoto hiyo wataifikisha mahali husika ili iweze kupatiwa ufumbuzi na kuwasaidia wakulima.

"Suala hili tutalifikisha kwa Waziri wa kilimo Hussein Bashe ili aweze kulifanyia kazi kwani chama chetu ni sikivu na kimelenga kuwaletea maendeleo wananchi wake hivyo tutahakikisha suala hili linafanyiwa kazi". Amesema katibu Peter.

Nao wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo Theopista Mhagama pamoja na Emmanuel Mgaya waliwataka wananchi kuendelea kujenga imani kwa chama hicho kwani serikali ya awamu hii imelenga kushughulika na kero zote ambazo ni kikwazo kwa wananchi.

Hata hivyo kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema alikwisha fuatilia jambo hilo kwa NFRA ili kujua sababu ya usitishwaji huo na kupewa majibu kuwa limesitishwa kutokana na wakulima wengi kupeleka mahindi yao hivyo wanahitaji kufanya utaratibu kwanza wa kuwalipa wananchi hao ndipo waendelee na zoezi la ununuzi hivyo anatumaini kupitia chama hicho jambo hilo litaenda kuhimizwa.

" Leo mmewasilisha changamoto hii kwa wenye Ilani ya uchaguzi ambao kinawapenda wakulima hivyo najua kupitia maandishi yao yenye wino wa kijani jambo hili litamfikia mama yetu kwa urahisi na soko hili la mahindi litakwenda kufunguliwa". Amesema Kamonga.TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments