Mapokezi ya Magdalena yanoga Arusha

ARUSHA; Mwanariadha wa Tanzania Magdalena Shauri, aliyeibuka nafasi ya tatu kwenye mashindano ya riadha ya Berlin yaliyofanyika Berlin, Ujerumani mwishoni mwa wiki, tayari amewasili nchini.

Mwanariadha huyo ambaye kutokana na kushika nafasi hiyo amepata tiketi ya kushiriki kwenye michuano ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa mwakani, amewasili Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) na kisha kufanyiwa hafla fupi ya mapokezi ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella.

Magdalena alitumia saa 2, dakika 18 na sekunde 40 kushika nafasi hiyo akiwapiku wanariadha wengine wa daraja la kidunia kwenye mashindano hayo.

Akitoa shukrani mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, mwanariadha huyo amesema wanawake wana uwezo wa kuinua michezo na vipaji vya aina mbalimbali nchini, ikiwemo kuitangaza Tanzania nje ya nchi kupitia riadha.

Magdalena sasa anaungana na wanariadha wengine wakubwa wa Tanzania ambao wamewahi kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa miaka ya karibuni.

Miongoni mwao ni mwanariadha Alphonce Simbu ambaye amewahi kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali kama kushika nafasi ya tano kwenye mashindano ya Olimpiki mwaka 2016, lakini pia kuwa mshindi kwenye mashindano ya riadha ya Mumbai, India mwaka 2017.

Mwanariadha mwingine maarufu wa Tanzania, Gabriel Geay, anafahamika kwa kuweka rekodi mbalimbali kimataifa, ikiwamo kumaliza nafasi ya pili kwenye mashindano ya riadha yaliyofanyika Boston, Marekani.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments