OFISI ya Waziri Mkuu kupitia taasisi ya kusaidia vijana sekta ya kilimo cha umwagiliaji imemteua mwekezaji wa kiwanda cha kuchakata na kusindika mafuta ya alizeti wilayani Rorya Wilfred Nyihita kuwa mlezi wa vijana Mkoa wa Mara.
Hafla ya kumsimika Mlezi wa Vijana kupitia Taasisi ya Tanzania Youth Agro Irrigation Develoment Network Programme imefanyika mjini Musoma katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mara ambapo Wilfred Nyihita na Uongozi wa Taasisi hiyo wametiliana saini ya makubaliano kwa lengo la utekelezaji utakao anza mwaka huu 2023.
Zoezi hilo pia lilihudhuriwa na wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya, maafisa Kilimo, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, wanasiasa, wakulima na taasisi za kijamii.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Afisa Kilimo Mkoa wa Mara Lazaro Butilikwa amesema jitihada za serikali ni kuhakikisha vijana wanapata mitaji ya kilimo kupitia mikopo ya asilimia nne inayotolewa na halmashauri za wilaya iliwemo kupewa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa kwenye maeneo yao.
Akizungumza baada ya kusimikwa rasmi kuwa mlezi wa vijana Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda cha kuchakata na kusindika mafuta ya Alizeti Nyihita Sunyfolwer Wilfred Nyihita amemshukuru Rais
Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango wa programu ya kuwajengea uwezo vijana katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mkoa wa Mara unahitaji kuwa na vijana wenye mtazamo na maono yenye tija ili kuenzi muasisi wa taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere ambaye alikomboa taifa kwa wakoloni na kuhimiza jamii kuwa kilimo ni uti wa mgongo.
Nyihita ameihakikishia Serikali Kuu kusimamia kikamilifu mpango wa kuwezesha vijana kuimarisha kilimo chenye tija ili baada ya muda mfupi Mkoa wa Mara uonyeshe mapinduzi ya kijani kuwa wa mfano kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuwa vijana wengi wamesoma na wamepania kujiajili kupitia kilimo chenye tija ili kuondokana na tatizo la upungufu wa chakula zaidi ya laki mbili kila mwaka
Baadhi ya vijana wa Mkoa wa Mara wameishukuru serikali kuanzisha programu hiyo ambayo itasaidia kuwakomboa vijana kupata ajira kupitia kilimo.
0 Comments