Mtwara, Lindi matumaini kibao ziara ya Samia

WAKUU wa mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na wananchi wao, wamesema wana imani ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan itakuwa na manufaa makubwa.

Rais Samia kesho anatarajiwa kuanza ziara ya siku tano katika mikoa ya Mtwara na Lindi, ambako atakagua miradi ikiwamo hospitali, bandari, kiwanja cha ndege, chujio la maji na barabara.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Ahmed Abbas amesema ziara ya Rais Samia italeta hamasa kwa wananchi hivyo kukuza uchumi.

Abbas alisema wananchi wa Mtwara wanajivunia kutembelewa na Rais Samia na anaamini kiongozi huyo ataacha alama kwa wananchi katika mkoa huo.

“Rais atakuwepo mkoani kwetu kwa takribani siku nne, ni jambo la kujivunia sana na sisi tunajiandaa kumpokea. Maandalizi yanakwenda vizuri, nawaomba wakazi wa Mtwara wajitokeze kwa wingi kumlaki Rais popote atakapopita akisimama kuongea nao wamsikilize,” alisema Abbas alipozungumza na HabariLEO jana.

Aliongeza: “Atakuja kuzindua miradi na ikimpendeza anaweza kutuongezea miradi mingine, tunamsubiri na tunaamini ziara yake itatuachia mambo makubwa yenye manufaa.”

Katika ziara hiyo, Rais Samia anatarajiwa kuzindua Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyopo Mikindani katika Manispaa ya Mtwara. Ujenzi wa hospitali hiyo inayotarajiwa kuhudumia wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma umegharimu Sh bilioni 15.8.

Aidha, Rais Samia pia anatarajiwa kuzindua chujio la maji Mangamba, na atakagua uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara na uzinduzi wa barabara za mkoa huo ikiwamo ya Mtwara – Mnivata.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack alisema Rais Samia atafanya ziara mkoani humo kuanzia Septemba 17 hadi 19, mwaka huu, akikagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo katika sekta ya afya, elimu na uchukuzi ikiwamo bandari ya uvuvi.

Telack aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake mjini Lindi jana kuwa Rais Samia atatembelea wilaya za Liwale, Nachingwea, Kilwa na Lindi.

Alisema Rais Samia ataweka mawe ya msingi ya Hospitali ya Rufaa iliyogharimu Sh bilioni saba, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya masomo ya sayansi inayogharimu Sh bilioni nane na mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi inayogharimu Sh bilioni 280.

Telack alisema ujenzi wa bandari ya uvuvi inayojengwa wilayani Kilwa umefikia asilimia 25. Alisema wilayani Nachingwea, Rais Samia atakagua wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), na pia atafika wilayani Ruangwa kuzungumza na wananchi.

Pia Rais Samia atazungumza na wananchi katika uwanja wa michezo wa Ilulu katika Manispaa ya Lindi.

Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Mtwara, Seif Chilumba amesema wananchi katika mkoa huo wanafarijika kutembelewa na Rais Samia.

“Kwa kweli sisi tunamshukuru sana Mheshimiwa Dk Samia, kuja kwake tunategemea kwamba atatia nguvu zaidi miradi ya wananchi na wananchi, tupo tayari kuipokea na kuisimamia kwa maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara na nchi nzima,” alisema Chilumba.

Mkazi wa Mtwara Mjini, Shilinde Shija amemkaribisha Rais Samia na kueleza kuwa wananchi wamepata fursa ya ajira kutokana na maboresho katika Bandari ya Mtwara hasa kutokana na usafirishaji wa saruji kutoka Kiwanda cha Dangote.

Saruji hiyo inasafirishwa kwenda Zanzibar, Comoro, Zambia, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mtaalamu wa tiba za viungo, Samson Mkawe amesema ziara ya Rais Samia Mtwara itakuwa na faida kubwa kutokana na uwekezaji wa kimkakati uliofanywa na serikali mkoani humo.

Mkawe alisema serikali imewekeza katika sekta ya afya ukiwamo ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini na imeimarishwa huduma za bandari ukiwamo upanuzi wa Bandari ya Mtwara.

“Anakuja kukagua miradi mingine mingi ambayo kupitia serikali yake umefanya imekuja kuleta manufaa makubwa kwa wananchi tukianzia uwekaji wa viwanda vidogovidogo, shughuli mbalimbali za kilimo, barabara pamoja na kwenye upande wa elimu pia,” alieleza Mkawe.

Mkazi mwingine wa Mtwara, Amani Mtepa alisema wanatarajia ziara ya Rais Samia itafungua fursa nyingi katika mkoa wao ikiwa ya uzalishaji wa gesi na usafirishaji wa korosho kupitia Bandari ya Mtwara.

“Tumesikia kauli za viongozi kwamba msimu wa mwaka huu korosho zetu za wana Mtwara zitasafirishwa kupitia bandari yetu ya Mtwara kwa hiyo ujio wa Rais tuna imani kubwa hili linakwenda kufanikiwa kwa asilimia 100,” alisema Mtepa.

Aliongeza: “Wana Mtwara tuna furaha kubwa sana, tunamkaribisha Rais wetu, tunamwambia tunampenda, aje ajisikie yupo nyumbani. Karibu sana Mama Samia Suluhu Hassan, wana Mtwara tunakupenda sana.”

Naye Asma Selemani alisema anaamini ziara ya Rais Samia itamaliza changamoto zinazowakabili ikiwamo ya kukatikakatika kwa umeme, kama ambavyo anaamini mkazi mwingine, Justin Bilali.

Mkazi mwingine wa Mtwara, Said Ahmad alisema anaamini Rais Samia ameelezwa changamoto nyingi za mkoa huo hivyo ameamua aende zifanyiwe kazi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments