Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa - MNEC, YOHANA MSITA amesema serikali inatambua mchango wa Machifu wa Makabila mbalimbali katika kuisaidia serikali kuwaletea maendeleo wananchi kwa kutoa maelekezo ya shughuli za kijamii na kiutamaduni.
MSITA alisema hayo Wilayani Ikungi mkoani Singida katika sherehe za kutimiza mwaka mmoja tangu Chifu wa Kabila la Wahijiu THOMAS MGONTO asimikwe kuwa Chifu wa Kabila hilo.
Alisema kuwa machifu wakishirikiana na serikali vizuri watasaidia kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kuwahimiza kufanya kazi kwa bidii na juhudi kwa miongozo inayotolewa na serikali.
Aidha MSITA aliwataka wananchi kupuuza Mila na Desturi za mataifa ya nje, ambazo zimekuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Kwa upande wake Chifu wa Kabila la Wahijiu Wilayani IKUNGI mkoani Singida THOMAS MGONTO amelaani vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na kusema kufanya hivyo ni kinyume na mila na desturi za kiafrika.
Alisema wao kama machifu wataendelea kuhakikisha mila na desturi za kiafrika zinafuatwa ili kuondoa momonyoko wa maadili katika jamii.
Chifu MGONTO alisema tuendeleze mila zetu kwa kuzilinda na kuziendeleza kwa kizazi cha sasa na kijacho, hata kwa wageni wanaokuja nchini waone zinafaa na kuzipeleka katika nchi zao.
Baadhi ya machifu walioshiriki katika sherehe hizo walisema wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi.
0 Comments