KAMPENI ya mtaa kwa mtaa ya uelimishaji jamii kutambua madhara ya vitendo vya rushwa imewafikia watu 12,671 mkoani Kigoma ambapo wamepatiwa elimu ya kujua madhara ya vitendo vya rushwa sambamba na wananchi hao kutoa taarifa kuhusu tuhuma za uwepo wa vitendo vya rushwa kwenye maeneo yao.
Mkuu wa dawati la elimu kwa Umma Takukuru Mkoa Kigoma, Leonida Mushema amesema hayo wakati akitoa taarifa yake ya utendaji kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Aprili hadi Julai mwaka huu.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa niaba ya kamanda wa Takukuru mkoa wa Kigoma,Stephen Mafipa alisema kuwa katika kipindi cha miezi hiyo mitatu maafisa wa Takukuru mkoa Kigoma walitembelea kata 14 za wilaya sita za mkoa wa Kigoma na kufanya vikao na wananchi ambapo jumla ya kero 208 ziliibuliwa.
Afisa huyo wa dawati la elimu kwa umma alisema kuwa katika kero hizo zilizoibuliwa kero 137 zimetatuliwa huku kero 71 zikiendelea kufanyiwa kazi ambapo alibainisha kuwa Taasisi hiyo ilipokea pia malalamiko 65 kati yake 28 yanayohusu tuhums za rushwa na 37 yasiyohusu tuhums za rushwa na kwamba malalamiko hayo yalifanyiwa kazi na ushauri kutolewa kwa walioleta malalamiko hayo.
Katika hatua nyingine Mushema alisema kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoa wa Kigoma inachunguza miradi miwili ya maendeleo kati ya miradi sita waliyokuwa wakiifuatilia yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7.
Mkuu huyo wa dawati la elimu kwa Ummanalisema kuwa miradi hiyo miwili inayochunguzwa ina thamani ya zaidi ya sh.milioni 43 na kwamba hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuonekana kuna mapungufu katika miradi hiyo ambapo mradi mmoja kati ya miradi hiyo sita walitoa ushauri kwa wahusika na marekebisho yamefanyika.
0 Comments