Watalii wakoshwa na tamaduni za asili

IRINGA:Watalii wanaokwenda au kutoka katika Hifadhi ya Taifa Ruaha,mkoani Iringa wamedaiwa kufurahia utalii wa utamaduni unaofanywa na vikundi vya kijamii ikiwemo ngoma, nyama inayochomwa kiasili na hata mavazi ya asili.

Vikundi hivyo vimeanzishwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii nchini kupitia mradi wa Kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii Nyanda za juu Kusini (REGROW) ambapo vimezisha mazao mapya ya Utalii kama vile ngoma za asili,vyakula vya asili, bidhaa za kiutamaduni kwa lengo la kuwainua wananchi kiuchumi pamoja na ulinzi wa maliasili nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi wa jamii ya kabila la Kimasai, Madicini Matayani, amesema watalii wanapoenda au kutoka katika Hifadhi ya Taifa Ruaha wanapitia kwenye vikundi vyao na kufurahia utalii wa kiutamaduni hususani ngoma, nyama inayochomwa kiasili, Mavazi ya asili nk.

Matayani ameongeza kuwa kutokana na fedha wanazozipata kutoka kwa Watalii maisha ya familia zao yamebadilika na sasa wanamiliki nyumba za kisasa, wanasomesha watoto, wananunua chakula cha uhakika na kuchangia katika uchumi wa nchi.

Wanufaika wengine wa Mradi kutoka Kikundi cha Tembo Pilipili kijijini hapo wameeleza kufurahishwa na mradi huo kwani kwasasa wameweza kusaidia kuimarisha shughuli za uhifadhi pamoja na kuwa marafiki wa Wanyamapori kwa kuandaa njia rafiki za kudhibiti Tembo kuingia katika makazi ya watu na kuharibu mazao yao kupitia mbinu za asili.

Naibu Msimamizi wa Mradi wa REGROW, Blanka Tengia amebainisha kuwa, mradi huo unatekelezwa kwenye Hifadhi nne, ambazo ni Hifadhi ya Taifa Ruaha, Hifadhi ya Taifa Nyerere, Hifadhi ya Taifa Mikumi na Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa na kuwa REGROW umekusudia kuimarisha uhifadhi wa Ikolojia na kuwezesha jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments