WAZIRI WA KILIMO AFAFANUA BEI YA PAMBA , AONYA WAPOTOSHAJI

 WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe ameeleza kwa kina kuhusu bei ya zao la pamba ambayo yenyewe inatokana na bei ya soko la dunia huku akitumia nafasi kuwaonya baadhi ya wanasiasa kuacha kuingiza siasa kwenye kilimo.

 Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wakizungumza na Wahariri kuelekea Mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika,  Waziri Bashe ametumia nafasi hiyo kuzungumzia bei ya pamba baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi.

Sababu za  kutoa ufafanuzi huo ni baada ya baadhi ya wanasiasa kudai kuwa bei imeshuka kwasababu ya baadhi ya viongozi akiwemo Mwenyekiti wa bodi ya Pamba ni mfanyabiashara.

Akielezea hilo Waziri Bashe amesema amesikia upotoshaji huo lakini ni vema ikafahamika wanachoweza kusimamia wao katika zao la pamba ni uzalishaji na  ubora lakini inapokwenda sokoni huko inabaki bei ya soko la dunia ikoje kwa wakati husika.

"Niwaambie wanasiasa chakula sio siasa , ni maisha ya watu, ni uchumi wa watu,  ngoja nitaje bei ya pamba kuanzia mwaka 2012 kilo ya pamba ilikuwa Sh.660 mwaka uliofuata ikawa Sh.700,

Sh.750, Sh.1000, Sh.1200, Sh.1100 na mwaka 2020 bei ikawa Sh. 850 kwa kilo moja.

" Mwaka jana 2022 bei ya kilo moja ya pamba ilikuwa Sh.2000 na sasa ni Sh.1060.Sasa ni ipi ya bei nchi zinazotuzunguka , tukianza na nchi ya Zambia bei ya kilo ya pamba ni Sh.780 mpaka Sh. 800.

"Kenya Sh.900 na Burundi  Sh.700 wakati wastani wa bei ya pamba duniani ,  wastani wa bei ya dunia kwa leo ni senti 78 mpaka sent 88 au senti 89. Hii ndio bei ya pamba katika soko la dunia, " amesema Waziri Bashe.

Amefafanua changamoto iliyopo katika nchi yetu imejengeka dhana  mbaya wananchi wanaamini viongozi wa siasa, viongozi wa dini,  kwa hiyo ukiwadanganya wanakubali.

"Mtu anasema makao ya bodi ya pamba yako Dar es Salaam kwasababu kuna jengo la Pamba House.Nchi ambazo zinatuzunguka kama Zambia wanauza pamba Sh.780 lakini wananunua mbolea na mbegu wenyewe.

"Mkulima wa Tanzania anapewa ruzuku yambegu na mbolea,  hivyo akichukua fedha yake anaweka mfukoni yoye.Hivyo pamoja na hayo Serikali inachukua hatua ya kubadilisha uzalishaji wa pamba ili uwe wenye tija, " amesema.

Pia amezungumzia kuchelewa kulipwa kwa wakulima wa zao la Tumbaku ambapo amesema kiasi ambacho kimelipwa ni Dola za Marekani milioni 200 na ambazo hazijalipwa ni dola milioni 40.

Hata hivyo amesema kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika zao hilo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 60 mpaka tani 120, 000 lakini na bei nayo imepanda.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments