Dk Mwigulu achangia Sh milioni 15 shule ya KKKT Iringa

WAZIRI wa Fedha, Dk Mwigulu Chemba ametoa fedha taslimu Sh milioni 15 kuchangia awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule ya awali na msingi inayojengwa na Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa katika kituo chake cha Huruma Center.

Shule hiyo ambayo hadi kukamilika kwake itatumia zaidi ya Sh bilioni 1.7 itawanufaisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo watoto yatima na waliofanyiwa ukatili kijinsia.

Pamoja na mchango wa Dk Nchemba, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Salim Asas, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Daudi Yasini, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego, wabunge na madiwani wamejitokeza katika harembee ya ujenzi huo iliyowezesha zaidi ya Sh Milioni 350 kati ya Sh Milioni 537 zinazohitajika katika awamu hiyo ya kwanza, kupatikana.

Harambee hiyo iliyofanyika katika kituo hicho cha Huruma Center iliongozwa na Naibu Waziri wa Tamisemi Deogratias Ndejembi aliyemwakilisha Dk Nchemba.

Huruma Center ni kituo ambacho pia kumekuwa kikipokea watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwamo ubakaji na ulawiti kwenye jamii wanazoishi.

Akilipongeza kanisa hilo kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita zinazolenga kuhakikisha watanzania wote wanapata elimu bila ubaguzi wa aina yoyote, Ndejembi alisema;

“Taarifa ya harambee hii nitaifikisha kwa Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan na nina imani ataweka mkono wake ili kuwasaidia kufanikisha ujenzi huu.

Ndejembi alisema licha ya serikali kuwekeza katika ujenzi wa madarasa na shule mpya, bado kuna umuhimu mkubwa wa kujenga shule maalumu mpya na kuziboresha zile zilizopo.

“Tumewaona hawa watoto, wameimba wimbo ambao ujumbe wao umetugusa, hivyo ni jukumu letu kuwasaidia na kuwafanya waishi vizuri kama watoto wengine,” alisema Ndejembi.

Awali Aksofu wa KKKT, Dayosisi ya Iringa Dk Blaston Gavile alisema wanajenga shule hiyo ili kuwanusuru watoto ambao imekuwa vigumu kusoma shule za kawaida baada ya kuathirika kisaikolojia kutokana na ukatili waliofanyiwa.

Aksofu Gaville alisema; “Kwa hakika watoto waliofanyiwa ukatili wanapaswa kulindwa. Ukatili kwa watoto ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na unaweza kuathiri maisha yao kwa muda mrefu hivyo tumeamua kuwajengea shule ili wasome mazingira wanayoishi.”

Alisema lengo kubwala kujenga shule hiyo ni kuwawezesha watoto hao walindwe na kusaidiwa kisaikolojia ili wafikie ndoto zao na hatimaye waishi maisha ya furaha na amani.

Kwa upande wake Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Profesa Owdernburg Mdegella ameitaka jamii ifike hatua na iseme basi kuhusu ukatili kwa watoto.

“Hili ni jukumu letu viongozi wa dini tuisaidie jamii, huu ukatili na uchafu dhidi ya watoto unaoendelea lazima tuhakilishe tunakemea,” Alisema Profesa Mdegella.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema alishaongea na watoto walio kwenye kituo hicho na kujua changamoto walizopitia ambazo zinawafanya wasaidiwe kutimiza ndoto zao.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments