Fatma Karume: Muungano haujaathiri Wazanzibari

 


MJANE wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume, Fatma Karume amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haujawaathiri Wazanzibari.

Alisema hayo nyumbani kwake Maisara visiwani Zanzibar wakati anazungumza na waandishi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

Fatma akasema tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964, hajaona kama muungano umewaathiri Wazanzibari kwa namna yoyote.

Anasema Watanzania hasa Wazanzibari wanapaswa kuuenzi, kuupenda na kuunyenyekea muungano huo kwa kuwa ni kiungo kizuri kati yao na wenzao wa Bara.

“Muungano ni kiungo chetu, na kiungo chenyewe ni kizuri sana, kimetutoa mawazo mabaya, kimetutoa ujinga, kila mmoja neema yake anaipata, kila mmoja kasafiri duniani anaona watu wanaishi vipi kwa ajili ya muungano,” anasema Fatma.

Anasema tangu muungano huo uanze, mpaka sasa haujasababisha hitilafu kwa Watanzania kwa kuwa waasisi wake, Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Rais Karume hawakuuanzisha kwa shinikizo la tamaa binafsi.

Kwa mujibu wa Fatma, waasisi hao waliuanzisha muungano kwa kuzingatia maslahi ya watu wao na pia walitaka Kenya na Uganda ziingie ili Afrika Mashariki (EAC) iwe moja kwa sababu hata Marekani ni muungano wa majimbo 50.

“Kwa hiyo waasisi wa muungano wetu wakaona hakuna maajabu kwa sisi waswahili kuungana, tukalinda watu wetu na nchi zetu, walikuwa na dhamira hiyo,” anasema.

Akaongeza: “Lakini katika kusikia na kuona kwangu katika kuunda huu Muungano, Nyerere akamwambia Karume wewe ndio utakuwa Rais wa huu muungano, lakini Karume akamwambia hapana, sitaki, bali wewe ndio utakuwa Rais wa muungano.”

Fatma anasema kuwa hoja zinazoibuka ikiwamo ya madai kuwa muungano unawameza Wazanzibari zimekuja baada ya Mwalimu Nyerere na Karume kufariki dunia.

Akasema baada ya waasisi hao wa muungano waliotengeneza mazingira mazuri ya muungano kutokuwapo baadhi ya watu wakaanza siasa za kupakana taka.

Kutokana na hilo, Fatma alisema yeye anauona muungano bado haujaharibika japo kuna wakati baadhi ya mambo yalikuwa yanawaudhi Wazanzibari kutokana na ukweli kwamba Zanzibar ni nchi na Tanzania Bara ni nchi.

“Tulikuwa tunapata misaada kutoka nje kwa mfano, sasa hapa kulikuwa na kasma inaletwa hapa kwa ajili ya kusaidia nchi yetu lakini ulikuwa unapita ukiritimba, ikawa inawaumiza wengine,” alisema.

Jambo analosema Fatma lilikuwa miongoni mwa hoja za muungano na nyingi tayari zimefanyiwa kazi.

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia vikao hoja 25 zimejadiliwa na hadi sasa 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya Hoja za Muungano.

Dk Jafo alisema mwaka 2010 hoja mbili zilipatiwa ufumbuzi, mwaka 2020 hoja tano zilipatiwa ufumbuzi, mwaka 2021 hoja 11 zilipatiwa ufumbuzi na mwaka jana nne zilipatiwa ufumbuzi.

Fatma alisema kwa kuwa yeye ni Mtanzania kutoka Zanzibar anauombea muungano uendelee kudumu kwa kuwa tunu hiyo ni heshima, stara na mwavuli wa Watanzania kwa mambo mbalimbali ya dunia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments