Geita wavunja mkataba na mkandarasi wa maji

GEITA; MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Geita (GEUWASA), imevunja mkataba na mkandarasi aliyekuwa na zabuni ya kujenga mradi wa maji katika Kata ya Bung’wangoko wilayani Geita mkoani hapa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Geuwasa, Mhandisi Frank Changawa amethibitisha taarifa hiyo na kudai hatua hiyo inatokana na utendaji usioridhisha wa mkandarasi.

Amemtaja mkandarasi aliyekuwa na zabuni ya mradi huo ni Kampuni ya KELLOGG Construction Limited, ambaye inadaiwa ameshindwa kutekeleza mradi kwa ufanisi na kwa muda uliopo kwenye mkataba.

Amefafanua, uamuzi umetolewa mbele ya timu ya menejimenti ya Geuwasa, ambayo ilifika eneo la mradi na kufanya ukaguzi wa maendeleo yake na kutoridhishwa na utendaji wa mkandarasi huyo.

Amebainisha mradi wa maji Bung’wangoko unatekelezwa kwa gharama ya Sh milioni 569 na utekelezaji ulianza Machi 27, 2023 na ulitarajiwa kukamilika Agosti 30, 2023 lakini mkandarasi huyo ameshindwa.

Amesema hatua za awali zilizochukuliwa baada ya muda wa zabuni kuisha mwezi Agosti mwaka huu walimuongezea muda, lakini aliendelea kusuasua na mpaka sasa mradi umefikia asilimia 15 pekee.

Mhandisi Changawa amesema baada ya kuvunja mkataba na mkandarasi huyo hatua inayofuata ni kuomba kibali kutka Wizara ya Maji, ili mradi huo uanze kutekelezwa kwa njia ya ‘Force Account’.

Diwani wa Kata ya Bung’wangoko, Thobias Ikanga amesema kukwama kwa mradi huo kumesababisha takribani wananchi 12,000 wa vijiji vitatu ndani ya kata hiyo kukosa maji safi na salama.

Ikanga amewaomba Geuwasa baada ya kuchukua hatua hizo wafanye juhudi thabiti kukamilisha mradi huo kwa wakati, ili kufikia suluhu ya kudumu ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mkurugenzi wa Kampuni ya KELOGI Construction, Heri Mwafute amesema kikwazo kikubwa cha mradi kwanza ilikuwa ni mchakato wa ulipaji Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuchukua muda mrefu.

Amesema pia kampuni iliomba kutengenezewa nondo maalum kutoka kiwandani ambazo zimechelewa kufika eneo la mradi, ambapo ziliwasili juzi na wapo tayari kukamilisha mradi iwapo wataridhia.

“Kazi za serikali tunazifanya sana, tuna uzoefu, si kwamba ni mara ya kwanza, hivyo tupo kwenye mazungumzo nao (Geuwasa) kama watakubali tupo t.ayari kukamilisha mradi, ” amesema

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments