Maji safi, salama Mtwara sasa asilimia 58

 


KAMPENI ya kumtua mama ndoo kichwani ni moja ya mikakati ambayo imesaidia kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Mtwara Mhandisi Hamisi Masindike amesema hayo wakati akiongea na mwaandishi wa habari hizi ofisini kwake.

“Kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ni moja ya mikakati ambayo imesaidia sana kuongeza upatikanaji wa huduma za maji safi na salama Wilaya ya Mtwara hasa vijijini,” amesema.

Amesema kwa sasa upatikanaji wa maji safi na salama Wilaya ya Mtwara umefikia asilimia 58.

“Upatikanaji wa maji umepanda, wakati RUWASA inaanzishwa 2019 upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 50 lakini kwa sasa tumefikia asilimia 58,” amesema.

Amesema RUWASA Wilaya Mtwara Vijijni ina jumla ya vijiji 197 na kati ya hivyo ni vijiji 52 tu ndivyo havina huduma ya maji safi kufikia sasa.

“Serikali imeweka mipango kuhakikisha vijiji ambavyo havina huduma ya maji ya RUWASA vinapata maji kabla ya kufikia mwaka 2025,” amesema.

Amesema mradi wa Makonde wenye thamani ya Sh bilioni 84 ambao unatekelezwa mkoani Mtwara utatoa huduma ya maji kwa vijiji ambavyo havina maji kwa Wilaya za Newala, Tandahimba, Nanyamba mji ikiwemo vijiji vya Mtwara Vijijini.

Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 inaelekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji umefikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo 2025.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments