Mavunde aitaka GGM kuimarisha mahusiano na jamii

 


GEITA: WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Geita Gold Mine(GGM) kuimarisha mahusiano na jamii inayozunguka mgodi ili wananchi waone manufaa ya uwekezaji huo katika eneo lao.

Waziri Mavunde ameyasema hayo mkoani Geita wakati akikabidhi basi kwa timu ya Geita Gold Football Club lililotolewa na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) kama sehemu ya ufadhili wao kwenye sekta ya michezo.

“Naipongeza serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia marekebisho ya sheria na kutungwa kwa kanuni za kuwajibika kwa jamii-Corporate Social Responsibility (CSR) ambayo leo yameweka msingi mzuri kwa makampuni kurejesha kwenye jamii.”Amesema Mavunde na kuongeza

“Niwapongeze GGM kwa ufadhili wa basi lenye thamani ya Sh milioni 500 kwa timu ya Geita Gold,naamini usafiri huu utachochea hari ya timu kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya NBC Premier League.”

Aidha, amewataka waongeze wigo wa kuimarisha mahusiano yao kwa jamii,kwa kuigusa jamii hii kimaendeleo katika nyanja mbalimbali zaidi ya hili la sekta ya michezo.

“Najua mna moja limebaki mbele yenu la ukamilishwaji wa uwanja wa Magogo,hili ni muhimu kukamilika mapema ili kuwafanya wanachi wa Geita wapate burudani ya michezo.”Amesema Mavunde

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella, amewataka wadau wa michezo mkoani Geita kuiunga mkono timu ya Geita ili iweze kufanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu.

Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mkuu wa GGML Terry Strong amesema Kampuni yake itaendelea kuimarisha mahusiano na jamii na kuchochea maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya michezo mkoani Geita.

Aidha, uongozi Geita wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi wa timu hiyo  Constantine Morandi aliishukuru GGM kwa ufadhili huo na kuwataka wachezaji na benchi la ufundi kuthamini ufadhili na uwe chachu kwa timu hiyo kufanya vizuri zaidi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments