Rais Samia aipatia Zambia hekta 20

ZAMBIA; Lusaka. RAIS Samia Suluhu Hassan ameipatia zawadi nchi ya Zambia ya hekta 20 katika eneo la Kwala mkoani Pwani, kwa ajili ya kurahisisha uchukuaji wa mizigo bandarini ikiwa ni siku yao ya kusherehekea kumbukumbu ya miaka 59 ya Uhuru wa nchi hiyo.

Pamoja na hayo amesema Tanzania imetengeneza mazingira mazuri ya ushirikiano na Zambia katika maeneo zaidi ya sita ikiwemo biashara, miundombinu na kujenga bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Zambia.

Maeneo mengine aliyotaja ni kwa pamoja nchi hizo kuhamasisha amani katika nchi za Afrika na dunia kwa ujumla na kuendeleza miradi iliyopo  ukiwemo wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).

Rais Samia aliyasema hayo wakati akihutubia katika sherehe za miaka 59 ya Uhuru wa nchi hiyo zilizofanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Lusaka, ambapo alikuwa mgeni rasmi wa sherehe hizo.

Alisema kupitia mipango ya Tanzania ya kurahisisha zaidi biashara kati ya nchi hizo mbili, serikali imetenga eneo hilo la Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo inayopelekwa Zambia.

“Zaidi ya hayo, Zambia itawezeshwa kwa muda mrefu zaidi wa kuhifadhi bila malipo mizigo ambao unaenda hadi siku 45. Hatua hii itapunguza msongamano na ucheleweshaji, na hatimaye kupunguza gharama za kufanya biashara nchini Zambia,” alisema.

Alisema Tanzania inatarajia hatua hiyo kwa hivyo,  itakuza biashara kati ya nchi hizo mbili na kutengeneza fursa zaidi za kibiashara kwa wananchi wa pande zote mbili.

“Hii ni zawadi kutoka Tanzania unaposherehekea uhuru wako,” alisema Rais Samia na kushangiliwa na wananchi wa Zambia,” amesema.

Mbali na hilo, Rais Samia alisema serikali pia imeanza uboreshaji wa mitambo ya Bandari ya Dar es Salaam ili kuhakikisha bandari hiyo inafanya kazi kwa ufanisi, kwa wakati na bila vikwazo katika shughuli zake.

“Ningependa kutoa wito kwa jumuiya ya wafanyabiashara nchini Zambia kuchangamkia fursa hii ya kipekee,” alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments