SAMIA AMLETA RAIS WA UJERUMANI NCHINI TANZANIA


#Ni baada ya ziara za kimkakati India, Zambia

#Ujerumani yavutiwa na utawala bora wa Tanzania chini ya Rais Samia

#Ushindi wa Tulia Ackson IPU ni matokeo ya diplomasia ya Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Ujio wa Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, nchini Tanzania na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Ujerumani ni ishara nyingine ya mafanikio makubwa ya Diplomasia ya Uchumi tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.

Rais Steinmeier yuko nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, baada ya Rais Samia kufanya ziara za kitaifa kwenye nchi za India na Zambia.

Katika ziara hizo za nje zilizokuwa na mafanikio makubwa, Rais Samia aliambatana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Tanzania kwa lengo la kuvutia mitaji, biashara na uwekezaji zaidi nchini Tanzania.

Akiongea Ikulu, Dar es Salaam, leo baada ya mazungumzo na Rais Steinmeier, Rais Samia amesema kuwa ziara hiyo ya kiongozi mkubwa wa Ujerumani itasaidia kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

"Leo nchi yetu imepiga hatua nyingine ya historia katika uhusiano wake na Ujerumani, tumepata heshima ya kumkaribisha Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Shirikisho la Ujerumani hapa Ikulu, Dar es Salaam, na hapa nchini Tanzania," Rais Samia alisema.

Katika mazungumzo ya viongozi hao wawili, Rais wa Ujerumani aliipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia kwa utawala bora na kuahidi kuleta wawekezaji kutoka Ujerumani kwa wingi nchini Tanzania kutokana na siasa zake zenye utulivu.

"Tumezungumza na Mheshimiwa Rais (Rais wa Shirikisho la Ujerumani Dkt. Frank Walter Steinmeier) ametupongeza kwamba Tanzania tunaonekana tumetulia kwenye utawala wa sheria na utawala bora na ndio maana wamevutika wafanyabiashara wa Ujerumani kuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji," Rais Samia alisema

Tanzania huagiza bidhaa za viwandani zenye thamani ya wastani ya zaidi ya Shilingi bilioni 600 kwa mwaka kutoka Ujerumani wakati inauza bidhaa kwa Ujerumani zenye thamani ya wastani ya zaidi ya Shilingi bilioni 100 kwa mwaka.

Tanzania huuza mazao ya kilimo kama kahawa, pamba, tumbaku, asali, nta, samaki na madini ya vito kwa Ujerumani. 

Rais Samia na mgeni wake wamezungumzia haja ya kuongeza biashara na uwekezaji zaidi baina ya Tanzania na Ujerumani.

Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia ameweka jitihada kubwa kwenye masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa na kuifanya Tanzania ing'are kimataifa.

Rais Samia amevutia viongozi wengi wakubwa duniani, ikiwemo Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, kufanya ziara nchini Tanzania.

Rais Samia pia amealikwa kwenye ziara za kitaifa kwenye nchi nyingi na kuhudhuria mikutano mikubwa ya kimataifa ambayo ameitumia kwa ufanisi kusukuma ajenda ya Diplomasia ya Uchumi.

Hivi karibuni, Rais Samia ameongoza kampeni ya kimataifa kuhakikisha kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, anachaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na hivyo kuleta heshima kubwa kwa Tanzania.

Aliporejea nchini kutoka kwenye uchaguzi wa IPU, Dkt. Ackson amemshukuru Rais Samia Kwa kumpigia kampeni na kuhakikisha anakuwa mshindi katika uchaguzi alishinda hivi karibuni.

"Nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ambae aliweka nguvu nyingi sana kwanza nafasi hii hauwezi kugombea kama Serikali yako haijakuruhusu kugombea nafasi hii ambapo amefanya kampeni kubwa sana na kuniambia kwasababu ni mambo ya kibungr," alisema Dkt.Tulia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments