Samia ataka kasi usambazaji maji

RAIS Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Maji na wakandarasi kuongeza kasi ya usambazaji maji ili kuwafikia wananchi kwa wakati.

Amesema hayo Oktoba 17, 2023 wakati akizindua mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya Mji wa Shelui katika hafla iliyofanyika kwenye Kijiji cha Kizonzo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

“Huu mradi umegharimu Sh bilioni 24.47 bado bilioni 16 zimebaki zinaenda kutumika katika usambazaji wa maji kwa maeneo mengine,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amezungumzia uanzishwaji wa matumizi ya mita kama suluhu ya malalamiko ya ubambikizaji wa gharama za maji kwa watumiaji.

“Kwa matumizi ya mita unatumia maji kadri ya malipo yako, pindi malipo yako yakiisha maji yanakata,” amesema Rais Samia.

Pia amezungumzia kuhusu namna serikali ilivyojipanga kuhakikisha kabla ya kufika mwaka 2025 Mkoa wa Singida na kila eneo ndani ya mipaka ya Tanzania litakuwa limeunganishwa na nishati ya umeme.

Rais Samia amemaliza ziara yake ya kikazi mkoani Singida, iliyodumu kwa siku mbili tangu Oktoba 15 hadi 17, 2023 na ziara hiyo inataraji kuendelea tena leo mkoani Tabora.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments