Shule 30 kunufaika na mpango wa chakula shuleni

 

KIGOMA: Zaidi ya shule  30 katika Wilaya za Kasulu na Kigoma mkoani Kigoma zimeanza kufaidika na mpango wa chakula shuleni kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) lengo likiwa ni kuunga mkono mpango wa serikali  wa chakula shuleni ili kuongeza ufaulu na mahudhurio shuleni .

Mkurugenzi na Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP), Sarah Godon-Gibson alisema hayo wakati akikabidhi kwa shule ya Msingi Kigadye wilayani Kasulu mkoani Kigoma mradi wa umeme Jua (Solar Panel) mradi uliotekelezwa kwa fedha kutoka serikali ya China ikiwa ni sehemu ya mradi huo wa kuimarisha mpango wa chakula shuleni.

Mkurugenzi huyo wa WFP alisema kuwa mpango wa chakula shuleni unalenga kuimarisha afya za wanafunzi waweze kusoma na kufaulu, kuwapa wanafunzi wa kike nafasi ya kupata masomo na kutekeleza usawa wa jinsia katika upatikanaji wa elimu.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian alisema kuwa nchi hiyo imekubali kufadhili mradi huo kutokana na umuhimu wa suala la elimu kwa watoto na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya nchi hizo mbili.


Balozi chen alisema kuwa China imetenga kiasi cha Dola bilioni nne kwa ajili ya kutekeleza mradi wa nishati safi na miradi ya teknolojia ambayo ni moja ya miradi inayolenga kukwamua uchumi wa watu kwa makundi sambamba na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa miradi inayoanzishwa kuwanufaisha kiuchumi watu hao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kigadye, Amiri Mohamed ameshukuru China na WFP kwa mradi huo ambao umewezesha kuzalishwa kwa umeme shuleni hapo ambao unatumika kuzalisha maji ya kisima ambayo yanatumika kwa ajili ya miradi ya bustani na matunda iliyoanzishwa shuleni hapo.

Kutokana na mradi huo mwalimu huyo alisema kuwa shule imeongeza uwezo kiuchumi kwa kuweza kuingiza kiasi cha Shilingi 50,000 kila wiki kwa kuuza barafu kama mradi wa shule, mboga na matunda ambayo pia yanatumika kwa ajili ya chakula bora kwa wanafunzi shuleni.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments