TAMWA – ZNZ YAOMBA MKAKATI WA KITAIFA KUBADILISHA TABIA KWA VIJANA

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinashauri kuandaliwa kwa mkakati wa kitaifa wa kubadilisha tabia za vijana ili kuwanusuru na kutumbukia katika vitendo vya udhalilishaji.

Kwa mujibu wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar kuanzia Julai mpaka Septemba, 2023 ni kwamba watu 24 wamekutwa na hatia mahakamani kwa kufanya makosa ya udhalilishaji na kupewa adhabu za vifungo (kwa Zanzibar huitwa vyuo vya mafunzo) ambapo asilimia 58.3 ni vijana wa umri wa 18-29.

Hii ni kwamba, vijana wamekua wakijihusisha sana na masuala ya udhalilishaji na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kuwabadilisha mawazo ili kutotumbukia katika majanga haya kwa maslahi yao, watoto na nchi kwa jumla.

Takwimu hizo pia zinaonesha watu ambao bado wapo mahabusu kesi zao zinaendelea ni 48 ambapo kundi hilo la miaka 18 hadi 29 pia linaongoza ambalo linafanya asilimia 54.

Tunaishauri Serikali kuandaa mkakati wa kuelimisha vijana kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo viwanja vya michezo, skuli lakini pia kutoa taaluma kwa wazazi na walezi jinsi ya kuwafahamisha watoto wa kiume namna ya kuheshimu watoto wa kike, wanawake na watoto kwa jumla.

Takwimu pia zinaonesha kuwa masuala hayo ya udhalilishaji yanawaathiri watoto zaidi ambapo katika matukio 157 kwa mwezi Julai hadi Septemba yaliyoripotiwa, watoto ni 122 sawa na asilimia 77 katika maeneo kadhaa hasa kubakwa, kakashifiwa na kulawitiwa.

TAMWA ZNZ pia inawashauri sana vijana kushtushwa na taarifa hizi na hivyo kujipangia mipango madhubuti ya kutokuingia katika vitendo hivi ikiwemo kuacha kufuata vishawishi, kutokuendekeza mihemuko na pia kujidhibiti dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao.

Ni vyema vijana wakaelewa kuwa katika vijana hao waliotiwa hatiani wengi wao wamehukumiwa kutumikia adhabu ya miaka 11 na zaidi hivyo kupoteza kipindi kirefu cha nguvu zao katika vyuo vya mafunzo badala ya kutumia kujipanga na maisha yao.

TAMWA ZNZ pia imefarijika sana na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa takwimu zinazoonyesha mgawanyiko wa umri wa waliofanya uhalifu ikiwemo makosa ya udhalilishaji.

Utoaji huu wa takwimu utasaidia kujua umri wa wafanyaji wa makosa mbalimbali na hivyo kuona jinsi gani nchi inaweza kujipanga katika kubadilisha tabia za makundi yaliyo hatarishi zaidi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

1 Comments