WIZARA YA ARDHI YASHIKA NAFASI YA KWANZA KUNDI LA WIZARA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekabidhiwa tuzo ya ushindi wa kwanza kwa upande wa kundi la Wizara iliyofanya vizuri katika kutekeleza uwezeshaji wananchi kiuchumi.


Tuzo hiyo iliyotolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) imekabidhiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa Waziri wa Ardhi Mhe. Jerry Silaa tarehe 2 Oktoba 2023 wakati wa ufungaji Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amewataka Viongozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuimarisha huduma za uwezeshaji ili kufikia malengo waliojiwekea na kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwezeshaji na kupunguza umaskini nchini.

Ametoa miezi mitatu kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini ambao bado hawajaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 wawe wameshaanzisha kabla ya mwaka 2024.

Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa alisema kongamano hilo linalenga kuongeza ufahamu wa wadau mbalimbali kuhusu dhana ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuwakumbusha majukumu waliyonayo katika kuwawezesha Watanzania.

Alisema malengo mengine ni pamoja na wadau kupeana uzoefu katika kutekeleza shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuzindua taarifa ya mwaka 2022/2023 ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo pia imejumuisha masuala ya ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika nchini.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi Tuzo ya ushindi wa kwanza kwa upande wa kundi la Wizara iliyofanya vizuri kwenye kutekeleza uwezeshaji wananchi kiuchumi Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa tarehe 2 Oktoba 2023 jijini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi Cheti cha ushindi wa kwanza kwa upande wa wizara iliyofanya vizuri uwezeshaji wananchi kiuchumi Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati wa kufunga Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma tarehe 2 Oktoba 2023.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments