Baraza UDSM kufuatilia ujenzi majengo 21

 

BARAZA la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) limejipanga kufuatilia utekelezaji wa mradi ujenzi wa majengo 21 ya chuo hicho chini ya Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi Elimu ya Juu (HEET).

Mwenyekiti wa baraza hilo, Balozi Mwanaidi Maajar amesema hayo wakati wa utiaji saini mikataba miwili ya usimamizi ujenzi wa majengo hayo yatakayojengwa kwenye maeneo mbalimbali ya Chuo Kikuu cha Dare es Salaam yaliyopo Dar es Salaam, Lindi na Zanzibar.

Amesema baraza litahakikisha utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa weledi na uadilifu ili kuhakikisha kuwa utekelezaji huo unakamilika kwa wakati, kulingana na muda uliowekwa .

“Tunasisitiza kuwa kila mmoja anayehusika kwa namna moja au nyingine katika utekelezaji wa mradi huu atimize wajibu wake kwa ufanisi inavyopaswa na kwa wakati unaotakiwa,” amesema.

Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema timu ya wataalamu katika chuo hicho imefanya kazi kubwa ya kuandaa michoro, kuiwasilisha kwa wadau na watumiaji wa majengo, kuifanyia marekebisho na kisha kupitishwa na baraza.

“Ni matumaini yetu kuwa majengo haya yatakidhi mahitaji yote muhimu ya wakati huu katika miundombinu ya kufundishia na kujifunzia. Wajenzi na wasimamizi wa ujenzi wahakikishe kuwa tunapata majengo bora na ya kisasa,” amesema.

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM upande wa Mipango, Fedha na Utawala Profesa Bernadeta Killian amesema chuo hicho kimetengewa kiasi cha Dola milioni 47.5 sawa na Sh bilioni 110 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa HEET kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Juni 2021 hadi Julai 2026.

“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatekeleza mradi kupitia fani za vipaumbele vya taifa ambazo ni pamoja na uhandisi na teknolojia; TEHAMA, mipango miji, uhandisi wa mazingira na teknolojia, kilimo na kilimo biashara, utalii na ukarimu.

Kwa upande wake Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET, Dk Liberato Haule amesema Mikataba itahusu washauri elekezi wawili ambao ni Arqes Africa Architects & Interior Designers Limited na Geometry Consultants Limited

Amesema Mshauri Elekezi Arqes Africa Architects & Interior Designers Limited atasimamia kazi 10 na mshauri Mwelekezi Geometry Consultants Limited atasimamia kazi 11 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments