CCM kumaliza miradi ya Hayati JPM

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kumalizia miradi yote iliyoanzishwa na Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli ikiwemo ujenzi wa msikiti, chuo cha fedha na mipango ambacho kinatarajiwa kuanza 2024 pamoja ujenzi wa hoteli ya kitalii yenye ghorofa tatu chato.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), itikadi na Uenezi, Paul Makonda alieleza hayo jana wakati wa akizungumza na wananchi katika uwanja wa stendi ya zamani wilaya ya Chato mkoani Kagera ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya Kanda ya Ziwa.

“Rais Samia ameniagiza kufika katika msikiti ulioanzishwa na Hayati Magufuli nitumie picha nimemtumia kasema ataujenga na miradi mingine ya hapa chato Rais Samia ameendelea kuitekeleza hivyo msikubali upotoshaji unasema na watu wasio na nia njema kuwa Rais Samia aendelezi,” alisema Makonda.

Alisema Rais Samia amendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa kasi nchini, ikiwemo ya hapa Chato ambapo ametoa fedha nyingi za maendeleo kutekeleza miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, ujenzi wa miundombinu.

Makonda alisema ataendelea kumsemea vyema vyema Rais Samia, kwa mema anayoyafanya nchini ikiwemo Chato ili kumuepusha na upotoshaji wa maneno ya watu ya kutoendeleza miradi hiyo iliyoachwa na Hayati Magufuli.

kiongozi huyo aliwapigia simu baadhi ya Mawaziri akiwemo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kujibu maswali ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa Chato.

Waziri wa afya Ummy Mwalimu alisema suala la hospitali ya Kanda ya Chato wameshatoa fedha za kuendeleza ujenzi, hivyo utekelezaji utaanza hivi karibuni na kuahidi kuwa watahakikisha wanapeleka mashine ya x-ray katika hospitali ya wilaya hiyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angela Kairuki alisema jengo hilo likikamilika litakuwa na ghorofa tatu, hivyo wanatamani kuona ujenzi huo unakamilika kwa wakati kunufaisha wananchi na kuleta maendeleo katika mkoa na nchini.

Naye Waziri wa elimu na mafunzo, Profesa Aldof Mkenda alisema kuwa wanaendelea kujenga Kampasi mbalimbali za vyuo katika mikoa hivyo ambapo kuna Chuo kitajengwa Chato Mjini huku wanaendelea na mpango wa ujenzi wa Tawi la Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Bukoba.

“Hapo Chato kuna chuo kimejengwa kinachoendelea kujengwa na tunatarajia kianze udahiri mwakani. Nitakuwa na ziara Bukoba hivi karibuni hivyo nitajitahidi nipite Chato kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu,” alisema Mkienda

Alisema tayari wamejenga chuo cha Veta Chato na sekondari ya ufundi mpya, hivyo kama kuna ardhi wapo tayari kuitumia vyema kwa ajili ya kuendelea kujenga shule na vyuo.

Aidha kiongozi huyo aliwataka Wakuu wa Wilaya na Mikoa wote kutenga muda wa kusikiliza kero za wananchi na kutatua changamoto zao zilizopo katika maeneo yao. Nakuwaonya Wakuu wa Wilaya na Wabunge kuacha kusigana bali washirikiene ili kufanikisha huduma za maendeleo kwa wananchi zinafikika kwa haraka.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Chato, Charles Mazuri alisema kuwa zipo shule mbili zilizojengwa kwa sh milioni 400 kila moja, lakini zote bado umaliziaji wake unasuasua ikiwemo tawi la chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kumuomba Makonda ayatolee ufafanuazi.

Awali Makonda alifika nyumbani kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Daktari John Pombe Magufuli Wilayani Chato Mkoani Geita na kuzuru kaburi lake na kuongoza sala fupi.

“Magufuli nakuahidi kama unaweza kusikia, Rais Samia Suluhu Hassan amenipa nafasi, nitakuwa msema kweli, nitakuwa mwaminifu kwa taifa langu na chama changu, na wewe huko uliko uendelee kuniombea ya kwamba ile kazi njema uliyotamani ifanyike katika taifa hili chini ya Jemedari na Kiongozi uliyemuachia nitakuwa sehemu ya kumsaidia na kumtia moyo Rais wangu Samia”

“Na kupitia yeye naamini Taifa litanufaika zaidi, asante kwasababu ulilipenda Taifa hili nasi tunakuahidi upendo huo ulishatuambukiza kwetu, tutaendelea kuwa Wazalendo na tutalilinda taifa hili na siku moja tukitwaliwa na sisi tukaache alama kama Magufuli ulivyoacha alama katika Taifa hili la Tanzania,” aliomba Makonda.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments