Chuo Kikuu Iringa wampa tuzo Rais Samia

RAIS wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan amepata tuzo ya Mlima Kilimanjaro inayotolewa na Chuo Kikuu cha Iringa kwa watu waliofanya mambo makubwa nchini.

Tuzo hiyo imepokelewa kwa niaba yake na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mahafali ya 26 ya chuo hicho yaliyofanyika leo, chuoni hapo mjini Iringa.

Katika mahafali hayo zaidi ya wanafunzi 1,900 wa fani mbalimbali wametunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali za masomo ikiwemo Astashahada, Stashahada, na Shahada za Uzamili.

Wengine waliowahi kupata tuzo hiyo ni pamoja na Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa na mkewe Anna Mkapa pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Tanzania, Venance Mabeyo ambaye kwa sasa ndiye Mkuu wa chuo hicho.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof Ndelilio Urio alisema chuo chao kimempa Dk Samia tuzo hiyo kikitambua kwamba ni mwanamke wa kwanza nchini kushika wadhifa huo mkubwa wa kuliongoza Taifa.

“Rais Dk Samia Suluhu Hassan alichukua madaraka hayo toka kwa mtangulizi wake nchi ikiwa katika hali ngumu na baadhi ya Watanzania wakiwemo wale wanaondekeza mambo ya mfumo dume hawakutegemea kama angeweza kuwa imara na kushika nafasi hiyo,” alisema.

Amesema Rais huyo amekuwa kiongozi wa mfano katika kusimamia mambo mengi yakiwemo yanayohusu utawala bora, uchumi, na utatuzi wa changamoto za kijamii ikiwemo ongezeko kubwa la wanafunzi wanaopata mikopo kutoka bodi ya mikopo.

“Chuo chetu ni mnufaika mkubwa wa wanafunzi wanaopata mikopo. Miaka mitano iliyopita tulikuwa na wanafunzi 376 tu wanufaika lakini hivi sasa tuna wanafunzi 2,834. Rais ameonesha usawa wa wanufaika wa mikopo katika vyuo binafsi na vya umma,” alisema.

 

Alimuomba Waziri Mkuu kuwafikishia salamu zao za pongezi kwa Rais, Prof Urio alisema juhudi za kiongozi huyo katika kukuza utalii nchini kwa kupitia filamu yake ya Royal Tour na mikakati mingine imeongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga kwa kozi ya utalii katika chuo chao.

Akizungumzia changamoto za chuo hicho, Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Liliani Badi alitaja moja ya changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa mabweni jambo linalowafanya wanafunzi wengi wapange nyumba nje ya chuo.

Amesema hatua hiyo imeleta madhara makubwa kwa wanafunzi wa kike ambao baadhi yao wamekuwa wakikutana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika nyumba wanazopanga na wengine kuingia katika ndoa za muda.

“Tunamuomba mheshimiwa Rais atusaidie ujenzi wa bweni letu la ghorofa kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema.

Akipokea tuzo hiyo na kuahidi kuifikisha kwa Rais, Waziri Mkuu alisema serikali inajivunia uwepo wa Chuo Kikuu cha Iringa kwa kuwa wahitimu wake wamekuwa wakionesha tija kubwa wanapoajiriwa katika sekta mbalimbali za umma na binafsi.

Aliwataka wahitimu wa chuo hicho kuendelea kutumia maarifa wanayopata kuchochea maendeleo katika maeneo wanayotoka.

“Kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia muwe wepesi pia kujifunza kuhimili ushindani wa soko la ajira na kuchangamkia fursa mbalimbali zitakzowafanya mjiajiri na kuajiri watu wengine” alisema.

Alikipongeza chuo hicho kwa kuanzisha Shahada ya masoko na ujasiriamali kwa vitendo ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

“Programu yenu ya kujifunza ujasirimali kwa vitendo ni jambo la kuigwa na vyuo kama mkakati wa kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira. Endeleeni kubuni na kutengeneza programu nyingi za kukabiliana na changamoto hiyo kwa vijana wetu wanaomaliza masomo yao kwa ngazi mbalimbali,” alisema.

Akizungumza changamoto ya upungufu wa mabweni Waziri Mkuu aliahidi kulifikisha ombi hilo kwa Rais, huku yeye mwenyewe akichangia Sh Milioni 10 kusaidia ujenzi huo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments