Japan yajitosa kambi ya wakimbizi Nyarugusu

DAR ES SALAAM: SERIKALI ya Japani  imetoa msaada wa  Dola za Kimarekani 500,000  sawa na Sh bilioni 1.250 kwa ajili ya kusaidia wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma.

Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa amekabidhi hundi ya fedha hizo kwa Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Mahoua Parums.

Misawa amesema nchi yake inatambua umuhimu wa  kulinda haki za binadamu na imekua ikifuatilia changamoto wanazokumbana nazo wakimbizi.

“Kwa niaba ya Serikali ya Japan nawasilisha mchango huu nikiamini kwamba utasaidia kwa kiasi fulani wakimbizi wapya kutoka Kongo kupata huduma za kibidamu zinazohitajika kama  huduma za kiafya, chakula hasa katika kipindi hiki ambacho bei za bidhaa zinazidi kupanda.”Amesema na kuongeza

“Tutaendelea kuunga mkono kazi zinazofanywa na UNHCR na serikali ya Tanzania kufungua milango na kuwasaidia wakimbizi wapya wa Congo katika kambi ya Nyarugusu.”Amesema

Akizungumzia msaada huo, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Mahoua Parums amesema kila siku Tanzania inapokea wakimbizi wapya 20 kutoka DRC Congo hadi sasa wapo zaidi ya 250,000 kitu ambacho ameeleza kuwa ni mzigo mzito kwa serikali ya Tanzania.

“Siku chache zilizopita nilikua Kigoma kwenye kambi ya Nyarugusu nikaongea na watoto na wanawake kutoka Congo, nikawauliza mbona wameacha miji yao, kazi zao wamekuja Tanzania, jibu walilonipa ni la kusikitisha, wamekimbia Congo ili kuokoa uhai wao.

“Hakuna anayependa kuwa mkimbizi,niliongea na kina mama wanalia, watoto wapo kwenye mazingira magumu lakini wanacheza wakiwa na matumaini mapya, wapo tayari kwa mapambano.”Amesema

Amesema, zinahitajika Dola milioni 150 kuhudumia wakimbizi waliopo nchini na kuziomba nchi nyingine kusaidia na kusema kuwa ana amini Tanzania itaendelea kufungua milango kwa wakimbizi.

Aidha, amesema fedha zilizotolewa na Japan zitaenda kusaidia kambi ya Nyarugusu kwa kujenga miundombinu kwa ajili ya wakimbizi wapya, vifaa tiba, neti za kuzuia mbu, wataalamu wa saikolojia, chakula na mavazi.

Wakimbizi wapya wanaokimbilia nchini  wakitokea  Kongo tangu Machi 5 mwaka huu,  ni kutokana na ongezeko la mashambulizii ya waasi wa kundi la M23 wanaokabiliana na majeshi ya serikali.

Mkoa wa Kigoma hadi sasa unahifadhi wakimbizi zaidi ya 250,000 kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Burundi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments