Kiruswa achangia Sh milioni 15 Ujenzi ofisi ya CCM Longido

Mbunge  wa Jimbo la Longido, ambaye ni Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa na marafiki zake wamechangia zaidi ya Sh milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya ofisi za cha hicho.

Katika harambee hiyo zaidi ya Sh milioni 72.2 zilikusanywa ikiwemo ahadi na fedha taslimu.

Harambee hiyo ilihudhuriwa na madiwani wote wa kata 18 za Jimbo hilo, viongozi wa jumuiya zote za chama ngazi ya kata na wilaya na viongozi wa chama na serikali ngazi ya kata na vijiji na Mwenyekiti na Katibu wa Chama Wilaya ya Longido ambapo kila kata ilikabidhi mchango wa Sh milioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya chama wilaya.

Dk Kiruswa alisema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa ofisi ya chama zilihitajika Sh milioni 49 na kwa makusanyo ya harambee iliyofanyika waliweza kuvuka malengo na aliiagiza kamati ya ujenzi kuhakikisha hadi kufika Disemba 31 mwaka huu awamu hiyo iwe imekamilika na Januari mwakani watendaji wote wa jumuiya na chama wawe ofisni.

Alisema awamu ya pili ya harambee ya Sh milioni 426 yenye kuhusisha vitega uchumi vya kuingizia chama mapato itakuwa ni pamoja na majengo ya biashara ikiwemo ofisi binafsi, maduka ya biashara na kumbi za mikutano na sherehe mbalimbali inatarajia kufanyika mara baada ya bajeti kuu ya serikali mwakani.

Mbunge huyo alisema chama kinahitaji fedha kwa ajili ya kujiendesha katika shughuli zake za kila siku hivyo ni wajibu wa kila mwana CCM kuhakikisha anachangia chama.

‘’Ninaiomba Kamati ya Ujenzi ya Ofisi za chama na vitega Uchumi vyake kuhakikisha imnalinda heshima yenu kwa kusimamia fedha zote za harambee zinafanya kazi kwa malengo yaliyokusudiwa’’alisema Dkt Kiruswa

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Ofisi za chama na vitega uchumi,Shamsia Ally alimwahidi Mbunge kuwa fedha za harambee zilizochangwa zitatumika kwa malengo sahihi na yaliyokusudiwa kwa asilimia mia moja na sio vinginevyo na awamu ya kwanza itakamilika vile vile kama tarehe ilivyopangwa .

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido,Saimon Oitesoi amemwakikishia Mbunge kuwa fedha zote za miradi katika wilaya hiyo ziko mikono salama na zitatumika kama zilivyokusudiwa na kwa wakati muafaka.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Longido,Papaa Nakuta aliwataka madiwani wa chama hicho kuwa kitu kimoja katika kukijenga chama na ikiwa ni pamoja na kushiriki katika harambee na kutoa kile kilichoazimiwa katika vikao yaani shilingi milioni moja kila kata.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments