KISWAHILI NYENZO MUHIMU KATIKA KUKUZA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA MALAWI

                  

Serikali ya Tanzania itaendelea kukuza na kuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili ili kuimarisha biashara inayovuka mipaka hususan katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo Malawi.


Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola alipokitembelea Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha nchini humo kwa lengo la kujadiliana na Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya kuanzisha ushirikiano baina na taasisi za elimu za Tanzania hususani katika kufundisha Lugha ya Kiswahili.

Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo hicho, Dkt. Kizito Elijah, Mhe. Balozi Kayola alisema kuwa, upo mwingiliano mkubwa wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi unaosababisha mahitaji makubwa ya kujifunza lugha ya Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano katika biashara.

Aliongeza kusema Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia na kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo mwezi Julai 2023 ikiwemo masuala ya ufundishaji wa Kiswahili nchini Malawi.

Kwa upande wake, Dkt. Elijah alisema kuwa, Chuo hicho kimepanga kuanzisha Kituo cha Lugha na kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania hususan Taasisi za Elimu na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili kutekeleza azma ya kufundisha Lugha ya Kiswahili chuoni hapo na kwamba chuo hicho kipo tayari kuanzisha ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania ikiwa ni pamoja na kubadilishana wakufunzi na wanafunzi.

Wakati huohuo, Mhe. Balozi Kayola ameitembelea Kampuni ya Kitanzania ya Bakhresa ambayo imewekeza nchini Malawi tangu mwaka 2003 katika viwanda vya uzalishaji Unga wa ngano, sabuni za kufulia na inatarajia kukamilisha kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kupikia mwezi Mei 2024.

Akiwa katika Kampuni hiyo Mhe. Balozi Kayola amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanyika na kuwahamasisha kuendelea kukuza wigo wa uwekezaji wa bidhaa mbalimbali nchini humo kwani mahitaji bado ni makubwa.

Kadhalika, Mhe. Balozi Kayola alipata fursa ya kukutana na Jumuiya ya Watanzania waishio katika Mkoa Kusini, Malawi ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuiwakilisha Tanzania nchini humo.

Katika mazungumzo yake na Jumuiya hiyo aliwaasa kuendelea kuwa wawakilishi wazuri wa nchi yao kwa kufuata sheria za nchi waliyopo ili kulinda taswira nzuri ya Tanzania.

Pia alisisitiza umuhimu wa wao kuendelea kujiandikisha kwenye Mfumo wa Kidigitali wa kuwatambua Diaspora (Diapora Digital Hub) ili iwe rahisi kuwaunganisha na fursa mbalimbali za biashara, masoko, na uwekezaji zilizopo nchini pamoja na kurahisisha utoaji wa msaada wakati wa dharura zinazoweza kuwapata katika nchi wanazoishi.

Mhe. Balozi Kayola alitumia fursa hiyo pia kuwajulisha kuhusu hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia huku akitaja Miradi mikubwa inayokamilishwa ikiwemo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR na miradi mingine kwenye sekta ya Kilimo, Biashara na Uwekezaji.

Vilevile, Mhe. Balozi Kayola aliwaeleza Diapora hao kuwa, Ubalozi upo tayari kushirikiana nao na kuwasisitiza kuwa huru katika kuwasilisha maoni, mapendekezo na ushauri kwa manufaa mapana ya Tanzania.

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akizungumza na Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi, Dkt. Kizito Elijah alipokitembelea Chuo hicho kwa lengo la kujadiliana na Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya kuanzisha ushirikiano baina na taasisi za elimu za Tanzania hususani katika kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi, Dkt. Kizito Elijah wakati wa mkutano kati yake na Balozi Kayola (hayupo pichani)
Mhe. Balozi Kayola akiagana na Dkt. Elijah mara baada ya kukamilisha mazungumzo baina yao


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments