‘Kuna pengo kubwa viongozi na wananchi’

 

MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema, lipo pengo kubwa kati ya viongozi wa serikali na wananchi, hatua inayosababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kutofahamika vyema.

Matinyi amesema hayo katika mkutano wake uliofanyika mjini Kibaha uliowahusisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge, Wakuu wa Wilaya, viongozi wa mkoa huo pamoja na wakurugenzi ambapo walielezea miradi iliyotekelezwa.

Amesema ni wajibu wa viongozi kuwaeleza wananchi miradi iliyotekelezwa na serikali, ili kuondoa pengo la wanachokiona wananchi na kinachofanywa na serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ambayo inatekelezwa nchini.

“Lipo pengo kati ya viongozi na wananchi, serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa ajili ya maslahi ya wananchi , lakini wananchi hawaelezwi michanganuo na mengine ambayo yamefanywa na serikali na ndo maana tukaanzisha mpango huu wa kuzunguka nchini nzima,”amesema na kuongeza:

“Tuliona lipo pengo ndo maana mkutano huu ni moja  ya mpango uliozinduliwa hivi karibuni jijini Dodoma  kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyofanywa na serikaii kwa kipindi cha miaka mitatu na itaendelea katika mikoa yote 26, ili taarifa za serikali ziwafikie wananchi,”amesema.

Matinyi amewataka viongozi wote wenye dhamana kusimamia fedha za utekelezaji wa miradi hiyo, ili iweze kuleta matokeo chanya kwa wananchi sambamba na kuwashirikisha kwa kila hatua kwenye maeneo husika.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, amesema katika kipindi cha miaka mitatu serikali ya mkoa huo imepokea Sh trilion 1.19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba hizo zimetumika kutekeleza miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu.

“Pamoja na miradi yote hiyo bado serikali ipo mbioni kuanza ujenzi wa upanuzi wa barabara  kuanzia Dar es Salaam-Chalinze-Morogoro, ambayo itaenda kuondoa msongamano sambamba na ujenzi wa barabara ya Chalinze-Utete, ambayo itafungua milango ya kiuchumi na maendeleo,”alisema

Katika mkutano huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Hemed Magaro aliishukuru serikali kwa namna ilivyotoa fedha za miradi ambayo imekwenda kutatua vikwazo kwa wananchi hususani katika eneo la delta.

Magaro alisema awali wananchi wa Mbwera walikuwa wanasafiri kilometa 90 kwenda kupata huduma za afya na wakati wa mvua walikuwa hawawezi kusafiri, hivyo ujenzi wa kituo cha afya katika eneo lao imeondoa tatizo lililokuwa linawakabili.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments