Makocha 21 wapigwa msasa Arusha

ARUSHA: Jumla ya makocha 21 wa kandanda wamemaliza kozi  ya awali yaani ‘Grassroots’ kwa ajili ya kufundisha vijana na watoto.

Mafunzo hayo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Royal, jijini Arusha, yameandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania kushirikiana na chama cha mpira wa miguu mkoa Arusha (ARFA)na kuendeshwa kupitia Mkufunzi wa TFF, Raymond Gweba.

Washiriki 20 ni kutoka Arusha na mmoja kati yao ni wa Mkoa wa Morogoro.

Mafunzo hayo ya siku sita yamefungwa rasmi na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA), Zakayo Mjema ambaye amewashauri washiriki hao kutafuta taasisi za soka, shule na timu za vijana na watoto kwenda kutoa maarifa na ujuzi walioupata.

“Badala ya kuweka vyeti vyako kwenye droo tumieni elimu mliyoipata kuwainua wachezaji wajao wa soka nchini kwa ngazi ya chini na hiyo , pia itatengeneza fursa nzuri kwenu, “alisisitiza Mjema.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Raymond Gweba amesema mafunzo hayo yalitolewa kwa nadharia na vitendo, kwa kutumia wanafunzi wa Shule ya Royal kama vielelezo vya kufundishia.

“Kumekuwa na matokeo chanya kutokana na kozi hizo kwani kwa sasa kuna vituo vingi vya mafunzo ya soka vinavyoanzishwa kote nchini,” amesema Gweba na kuongeza kuwa ni wakati muafaka wamiliki vituo vya michezo na mameneja wa shule waweze kuwasiliana na vyama vya soka vya mikoa ili kupatiwa walimu na wakufunzi wa soka wenye sifa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments