Maofisa uhamiaji mbaroni tuhuma za mauaji Kakonko

KIGOMA: POLISI mkoani Kigoma imewakamata maafisa wanne wa idara ya uhamiaji Mkoa wa Kigoma wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara wa Katoro Mkoa Geita mwenyeji wa kijiji cha Ilabiro Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Enos Elias  aliyeuawa akiwa kwenye mikono ya maafisa uhamiaji Wilaya ya Kakonko.

Taarifa kutoka chanzo cha kuamimika wilayani Kakonko kimeliambia HabariLeo  kwamba maafisa hao walikamatwa Ijumaa jioni na kuanza kuchukuliwa maelezo kuhusu kuhusika kwao na jambo hilo.

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Novatus Dawson amethibitisha kukamatwa kwa maafisa uhamiaji hao Kakonko na kwamba suala hilo lipo mikononi mwa polisi Mkoa wa Kigoma.

Kamanda wa polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu amethibitisha kukamatwa kwa maafisa uhamiaji hao wa Wilaya Kakonko na kwamba ni hatua za uchunguzi kujua ukweli wa kuhusika na kifo cha Enos Elias.

Makungu alisema kuwa bado maofisa hao ni watuhumiwa na ukweli utathibitika baada ya kufanyiwa mahojiano hivyo kwa sasa hakuna taarifa zaidi za kuelezea jambo.

Sambamba na hilo Kamanda Makungu amekataa kutaja idadi ya maofisa waliokamatwa wala idadi yao kwa maelezo isije kuingilia hatua za uchunguzi na kutaka watu wote wanaotaka taarifa wasubiri uchunguzi ukamilike na taarifa kamili itatolewa.

Mfanyabiashara huyo inasadikiwa kuuawa Oktoba 29 mwaka huu baada ya kukamatwa na maofisa uhamiaji Oktoba 27 kwenye kizuizi cha Kiomoka Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.

baada ya kukamatwa Mfanyabiashara huyo alilazwa kituo cha polisi Kakonko na tarehe 29 alichukuliwa na maofisa hao wa uhamiaji  ambapo taarifa zake hazikupatikana tena hadi polisi walipotoa taarifa kuwepo kwa mtu aliyezikwa akisadikiwa kuwa ni mfanyabiashara huyo wiki moja baadaye.

Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Kiganamo mjini Kasulu Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuwa jambo moja la kukamatwa kwa maofisa hao limetekelezwa lakini akataka kuwajibishwa kwa Mkuu wa Wilaya Kakonko na idara ya uhamiaji kutoa fidia kwa familia ya marehemu.

Post a Comment

0 Comments