Mikoa 3 vinara ukatili wa Kijinsia

 : MIKOA ya Mara, Kagera na Dodoma imetajwa kuwa kinara wa matukio ya ukatili ikiwamo vipigo, mauaji na ubakaji.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya siku 16 za Kupinga ukatili wa Kijinsia, Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) pamoja na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI), imeiangukia serikali kufanyia kazi mambo matano ili kutokomeza ukatili wa kijinsia katika mikoa hiyo na nchini kwa ujumla.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo Novemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa WiLDAF Dk Monica Mhoja amesema asilimia 40 ya vitendo vya ukatili inafanywa kwa mikoa hiyo kutokana na kukumbatia mila na tamaduni kandamizi.

“Tumefanya tafiti Mara, ndoa za utotoni bado zipo nyingi, mtoto miaka 14 analazimishwa kuolewa kwa baba mtu mzima, watoto wanapigwa mpaka kupasuliwa vichwa, wanazalishwa wakiwa na umri mdogo wengi upoteza maisha kwa vile via ya uzazi havijakomaa,”amesema Monica

Kufuatia hali hiyo wameiomba serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kutunga sheria mahususi ya kushughulikia maswala ya Ukatili wa kijinsia ili kupunguza vitendo hivyo kama ilivyoanishwa na Sheria ya mfano ya Jumuiya yaMaendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Model Law) ambayo Tanzaniani Wanachama na tulishiriki katika kuitengeneza.

Pia, wameiomba serikali kupitia Wizara yenye dhamana kuharakisha mchakato wa
utungaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili wa
Kijinsia (MTAKUWA II).

“ Vilevile serikali iwekeze bajeti ya kutosha itakayosaidia kamati zilizoundwa katika utekelezaji wa MTAKUWA kufanya kazi kwa ufanisi,”amesema

Ombi la tatu ni serikali kufanya mapitio ya kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa na uchakataji wa Takwimu za Ukatili wa Kijinsia ili ziweze kuoana kati ya watoa huduma hizo na kwamba hali ilivyo sasa mifumo ya watoa huduma wakiwemo Polisi, Ustawi wa Jamii, Afya, Mahakama haifanani na hivyo kusababisha mashauri mengi yakiendelea kwa kukosa ufumbuzi yakinifu.

Pia, wameomba kuharakisha wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1972 Sheria hiyoimewapa nguvu wanaume na familia kutumia mapungufu yaliyopo kama fursa kuwaozesha watoto na kupenya mkono wa sheria.

“Sheria hii imedogosha sheria zingine kama vile Sheria ya Elimu na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009. Ucheleweshaji wa mabadiliko ya sheria hii, umeendelea kusababisha watoto wakike kuolewa katika umri mdogo na kukumbana na ukatili wa kijinsia kwa sababu ya kushindwa kuhimili mikiki ya ndoa,”amesema Monica

Aidha, amesema wanatambua serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ipo kwenye mchakato wa kukusanya maoni ya wadau juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa. Hata hivyo, mchakato huo umechukua muda mrefu kufuatia maamuzi ya kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebeca Gyumi (Rufaa ya Madai Na. 204 ya mwaka 2017, Mahakama ya Rufani ya Tanzania Jijini Dar es Salaam), katika hukumu yake iliyotolewa
Oktoba 15, 2019.

Katika hukumu hiyo ilikiona kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa [Sura ya 29 ya Sheria za Tanzania, 2022] kuwa kinyume cha katiba na kuiamuru serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ndani ya mwaka mmoja. Hata hivyo sheria hiyo bado haijafanyiwa mabadiliko.

“Tunaomba serikali kupitia Wizara yenye dhamana kuimarisha Mwongozo na kuweka kanuni madhubuti zitakazo linda Wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji kwenye siasa wakati wa uchaguzi ili waweze kushiriki kikamilifu katika michakato yote ya kidemokrasia ikiwemo uchaguzi,”amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments