Mradi watafuta mwekezaji baada ya kukosa mkopo

MRADI wa kilimo wa Farm For the Future uliowekeza zaidi  zaidi ya Sh Bilioni 7.4 wilayani Kilolo mkoani Iringa unatafuta mwekezaji mbia wa kufanya naye kazi ikiwa ni matokeo yanayosababishwa na kushindwa kupata mikopo kwa wakati kutoka katika benki za kibiashara nchini.

Mradi huo unajishughulisha na uzalishaji wa mbegu za mahindi, umejikita pia katika kuzalisha maharage, karanga miti na viazi mbatata, vyote vikilimwa kibiashara.

Akizungumza kwa uchungu mbele ya Mwenyekiti wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Meneja Mradi wa shamba hilo la zaidi ya hekta 350, Osmund Ueland alisema juhudi zao za kupata mikopo kwa wakati kutoka katika taasisi hizo kwa ajili ya kuendeleza mradi huo zimekuwa zikigonga mwamba na kuathiri shughuli zao za uzalishaji.

“Tumepita katika changamoto kubwa katika benki hizo. Hatuelewi kwanini pamoja na kufanya uwekezaji huu mkubwa tunashindwa kupata mkopo kwa wakati ili nasi shughuli zetu za uzalishaji zifanyike kwa wakati ili kutokuwa na athari kwa pande zote mbili,” alisema bila kutaja kiasi cha mkopo na benki walizopeleka maombi yao.

Alisema wanatarajia serikali itawaunga mkono katika kushughulikia changamoto hiyo kwani ni habari njema kwa nchi baada ya kuanzisha mradi huo wa kilimo wenye lengo la kuongeza usalama wa chakula nchini.

“Kule kwetu Norway kwa miradi kama hii inaweza kupata fedha za mkopo kupitia mfumo wa Over Draft kama njia ya dharula ya kupata fedha haraka kwa kuzingatia masharti, riba na ada zinazohusika na huduma hiyo lakini hapa Tanzania imekuwa ngumu sana,” alisema.

Kutokana na mkwamo huo alisema wanalazimika kutafuta mbia ambaye watafanya naye kazi kwa makubaliano maalumu kama njia ya kuwawezesha kupata fedha za kuendeleza mradi wao na kufanya uzalishaji kwa kuzingatia kalenda ya kilimo.

Hata hivyo Ueland aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa mkopo wake wa vifaa vya kilimo ilioutoa kwa wakati kwa shamba hilo akisema utaboresha uwezo wa uzalishaji, kupunguza kazi za mikono, muda na nguvu za wafanyakazi.

Meneja Msaidizi wa shamba hilo lililoanza mwaka 2018, Grace Kimonge aliongeza kwa kusema; “Ili mpango huu ufanikiwe tunalazimika kuuza hisa ambazo gharama yake ni Sh 10,000 kwa hisa moja.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo ha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk Bilinith Mahenge ameahidi kuichukua changamoto hiyo na kwenda kuifanyia kazi.

“Angalau TADB imeonesha njia kwa kuwapa mkopo wa vifaa, kwahiyo tutakwenda kukaa na mamlaka zinazohusika ili kuona namna jambo hili linavyoweza kushughulikiwa kwa maslai ya pande zote mbili,” alisema.

Dk Mahenge alisema nchi inahitaji uwekezaji na RaisSamia Suluhu Hassan ameonesha utashi wa hali ya juu katika kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje hivyo ni wajibu wetu kupunguza au kumaliza kabisa changamoto zinazochelewesha au kukwamisha shughuli hizo za uwekezaji.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments