Soka la wanawake na unyanyapaa michezoni

 

TANZANIA ni mfano wa mataifa ya kuigwa yaliyopiga hatua kwenye soka la wanawake, kwa kushiriki Kombe la Dunia kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 17 nchini India mwaka 2022 na kufanikiwa kufika robo fainali kwa Afrika.

Na kwa upande mwingine nchi ikiwa imetwaa makombe ya Kanda ya Mashariki na Kati (Cecafa) na Kanda ya Kusini (Cosafa), kwa timu za umri kuanzia chini ya miaka 17, U-20 na Twiga Stars na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya Wanawake.

Pia klabu za wanawake zimeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanikiwa kufika nusu fainali ambayo ni kati ya timu nne za juu ikianza Simba Queens na sasa JKT Queens katika mashindano yaliyoanza Novemba 5-19 nchini Ivory Coast katika miji ya Korhogo na San Pedro yakishirikisha timu nane.

Pamoja na maendeleo hayo bado soka la wanawake linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kudumazwa na ukatili. Ukatili huu dhidi ya wanawake wanaocheza mpira wa miguu hujitokeza katika namna tofauti tofauti, inaweza kuwa wa kimwili, kingono au kifikra na inaweza kufanyika hadharani, faragha au mtandaoni na kutekelezwa na mpenzi au mtu mwingine yeyote.

Miongoni mwa sababu za ukatili kwa wachezaji wanawake hasa chipukizi kwa mujibu wa mahojiano na uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ni jamii kutojua haki ya wanawake kucheza soka na maana ya chapa wanayoibeba.

Hali ya kutojua maana ya chapa inasababishwa na wao kutojitambua namna ya kujiweka na ‘kujiuza’ katika jamii ili kuondoa unyanyapaa na kuwaita majina yasiyofaa.

Haya majina yasiyofaa kama ‘jike dume’ au ‘tomboy’ yanatoa taswira ambayo si sahihi inayowaumiza kisaikolojia na kukosesha hamasa kwa wasichana wengi wenye vipaji kujiunga na soka au kupata sapoti kutoka kwa wazazi na walezi.

Maneno ya unyanyapaa yaliyojengwa na utamaduni wa kumuona mwanamke kama kiumbe duni ni sehemu ya ukatili unaonyima uhuru wa mtu kufanya kinachostahili, anachokipenda au kukuza vipaji vyake kiuchumi katika utamaduni ambao unamuona mwanamke ni kiumbe wa hali duni.

Pamoja na ugumu unaowekwa kwa sababu za mifumo iliyopo katika jamii na wanawake wanaocheza mpira wa miguu kudhaniwa hawafai au wamekengeuka maadili, kuna mambo mengi yanayoweza kufanywa ili kubadili fikra na mojawapo ni kuiangalia chapa ya mchezaji katika soka la wanawake.

Mchezaji wa Simba Queens, Fatuma Issa  maarufu kama Fetty Dancer, amefanikiwa kujitambulisha kwa staili yake ya kuvaa hijab. Hili alilofanya ni jambo zuri na la muhimu kwani udhabiti wa jina lake na uharaka wa kutambulika kumemfanya kung’aa na kuwa mchezaji mwenye kuheshimika sana.

Kiukweli chapa inayofanikiwa pia ina wateja waaminifu ambao wako tayari kueneza habari kuhusu chapa hiyo kwa wateja wengine watarajiwa.

Katika kukabili unyanyapaa, Twiga Stars imeheshimisha wachezaji kwa kuwafanya wawe na mwonekano wa kike, wanasuka, wanavaa vizuri kama wanawake na hivyo kuwapa staha miongoni mwa jamii inayowazunguka wakiheshimu kazi ya soka wanayoifanya na kuipongeza.

Ukiangalia kikosi cha Twiga Stars kilichocheza na Botswana katika mchezo wa kufuzu Olimpiki 2024, wachezaji wote na viongozi wao walikuwa katika wajihi wa kike, hivyo kuondoa kabisa fikra za wazazi kwamba wasichana wanaofanya shughuli za soka, lazima wajinasibu kama wanaume na walakini katika mifumo yao ya utambuzi.

Kwa miaka kadhaa imekuwa taabu kushawishi jamii kutokana na chapa ya mdada kuwa mfano au ishara ya mafanikio kwa upande wa soka la wanawake kwa sababu za unyanyapaa uliopo miongoni mwa wazazi, walezi na wapenzi wa soka kutokana na namna baadhi ya wachezaji walivyojinasibu kuhusu wachezaji wanawake.

Wengi wanafikiri kuwa mwanamke kucheza soka ni kujifaragua, lakini maendeleo yaliyopo kwa baadhi ya wachezaji waliotangulia kunaanza kubadilisha mawazo na kuleta kiu kwa watoto wa kike na wazazi/walezi kuruhusu watoto wao wa kike kushiriki kucheza soka.

Pamoja na uzuri unaoanza kuonekana baadhi ya wachezaji wa kike, wadau wanadhani kwamba soka ni mchezo wa wanaume na kuwafanya baadhi ya wale waliojiunga kujinasibu onesha ‘uvulana’ zaidi, hivyo kuwaaminisha mashabiki kwamba kuna uharibifu wa tabia zilizoeleweka za wanawake katika kujiunga na soka.

Uharibifu huu wa kisaikolojia unastahili kufanyiwa kazi ili kuondokana na ukatili unaoumiza kwa wanaotaka kusakata kabumbu.

Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura anasema jamii inapaswa kujua kuwa chapa inatengenezwa, iwe ya mchezaji wa kike au wa kiume, hivyo wachezaji wenyewe ndiyo wenye fursa ya kuonesha wao ni chapa na ni chapa ya aina gani.

“Kwanza ni lazima tutambue kuwa tabia, wajihi na chapa inatengenezwa, iwe kwa mchezaji wa kike au wa kiume na haiwezi kutenganishwa na mafanikio, nidhamu na uadilifu,” anasema Wambura.

Wambura anakiri kuna changamoto kubwa ya udhamini kwenye mpira wa miguu wa wanawake na inatokana na kweli kuwa mpira wa miguu wa wanawake unatazamwa kama sehemu ya maendeleo, si chapa.

“Lakini TFF inaendelea kupambana kuhakikisha wadhamini wanakuja kutuunga mkono. Hivi sasa tuna udhamini wa Ligi Kuu ya Wanawake (Serengeti Lite Premier League- SWPL), ingawa hautoshi lakini unatoa mwanga kuwa huko mbele tutafanikiwa.”

Kufanikiwa huko kutaongeza hamasa na hivyo kuondoa fikra potofu kuhusu wanawake wanaoshiriki soka, kwani walezi na wazazi watatambua kwamba kuna faida katika jambo hilo na wala haliharibu mfumo wa familia na itikadi zake.

Kukubalika kwa chapa kutaleta unafuu mkubwa kwa wanawake na hivyo kuondokana na dhana potofu kwamba soka ni la wanaume na wanawake wanaposhiriki kuna walakini.

“Lakini pia kuanzia msimu huu, SWPL nayo inakwenda kuoneshwa kwenye televisheni. Hatua hii tunaamini itavutia wadhamini wengine si kwenye ligi tu, bali pia kwa klabu zinazocheza ligi hiyo,” anasema Wambura ambaye anaamini kwamba mafanikio ya soka la wanawake itaondoa kabisa dhana potofu zinazozunguka jamii, zinazozuia wanawake kusonga mbele katika soka la kulipwa.

Anasema katika kutafuta kuondoa dhana potofu kuhusu soka la wanawake, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), limeanzisha programu ya Guardians ambapo walezi watakuwa kwenye timu kwa ajili ya kuwalinda na kuwashauri watoto wanaocheza mpira wa miguu, lengo ni kuufanya mpira wa miguu kuwa mchezo salama katika maeneo yote.

Katika kuwapatia maendeleo ya kweli ya soka yenye wasifu unaondoa dhana potofu kuna haja kwa wachezaji kuwa na mameneja wa kuwasaidia kwani dunia ya leo, si kwa mpira wa miguu pekee bali kila nyanja inahitaji utaalamu, hivyo ili kutengeneza au kujenga chapa ni lazima mchezaji amtumie wakala au meneja kwa ajili ya kumpa mwongozo.

Mchezaji kazi yake kucheza na akili yote anatakiwa ailekeze uwanjani na kazi za nje ya uwanja zifanywe na watu wengine.

Ili kuondokana na dhana inayosababisha uharibifu wa kisaikolojia, Wambura anasema vyombo vya habari vinatakiwa kusaidia kuondoa fikra zisizo sahihi kuhusu wanawake na soka na kuonesha jinsi ilivyo vyema kwa wasichana na wanawake kushiriki katika mchezo wa soka wakiwa na udhabiti wa chapa na jina linalouzika.

“Vyombo vya habari haviwezi kujitenga na mafanikio. Mafanikio ya Serengeti Girls ya kucheza robo fainali ya Kombe la Dunia kulifanya vyombo hivyo viimulike timu hiyo,” anasema Wambura na kutoka hapo tunaona wachezaji wakipata fursa mbalimbali za kucheza klabu zenye maslahi makubwa zaidi.

Wambura anasema huwa wanawashauri wachezaji kuwa na uangalifu katika matumizi ya mitandao kwani inaweza kuwafanya wawe chapa au ikawaharibia kabisa, hivyo ni lazima mchezaji ajue au awe na utambuzi wa nini cha kuweka kwenye ukurasa wake na nini cha kutoweka.

Kwani akiweka kitu cha hivyo kitamuondolea sifa kama mchezaji na kufanya watu wengine kuona kwamba shughuli anayofanya anailazimisha.

“Bado kama mchezaji mwenye malengo anahitaji kuwa na mtaalamu wa kumshauri jinsi ya kuendesha mitandao yake ya kijamii.

“Bahati mbaya wengi hufungua mitandao ya kijamii ili kutafuta wafuatiliaji (followers) na jamii inapenda kusoma au kufuatilia vitu hasi! Huu ni mtego kwa wengi wanaotaka kutumia mitandao kujitengenezea chapa,” anasema Wambura.

Mdau wa soka la wanawake kutoka Arusha, Gloria Mbise anasema watu wengi wanawachukulia wachezaji wanawake kuwa na tabia za kiume jambo ambalo si kweli ila tu ni vile jamii ilizoea kuwa ni mchezo wa kiume ila ni mchezo wa watu wote.

Kuhusu kuwa chapa anasema ni mtu mwenyewe anavyojitambulisha kwenye jamii wengi wanajiweka tofauti kwa uvaaji, unyoaji na tembea zao na kusababisha kuonekana kama wa kiume na kuhofia tabia za mapenzi ya jinsia moja, hivyo wanatakiwa kuishi kama wasichana katika maadili na utamaduni wa Kitanzania ili kufuta dhana na hivyo kuzuia unyanyapaa na pia ukatili wa aina nyingine.

Anasema wakiweza kuwa na mwonekano wa kike kutaondoa dhana potofu kwani kuna minong’ono ipo na wengine wanawaona wanavyoishi wakati mwingine wanaonekana wakikaa kama wapenzi na kufanya jamii iwaone kama wana mahusiano ya jinsia moja.

Suala hili la minong’ono ya mapenzi ya jinsia moja kwa wachezaji wa kike, Wambura anasema suala hilo bado limeendelea kuwa minong’ono na kuwataka wadau wa mpira wa miguu wenye taarifa hizo kutoa ushirikiano na watazipokea na kuzifanyia kazi.

“Suala hili bado limeendelea kuwa minong’ono. Lakini si kwamba TFF hailifanyii kazi. Ukiacha taratibu za mpira wa miguu pia utamaduni wa kiafrika haukubaliani nalo. Bado wadau wenye taarifa hizi, TFF iko wazi kuzipokea ili izifanyie kazi,” anasema Wambura kwa sauti ya msisitizo.

“Tumepata mafanikio kwenye mpira wa miguu, ili kulinda mafanikio haya ni lazima tujenge mazingira ya kufanya watoto wengi zaidi wa kike wacheze mpira wa miguu.  TFF ikibaini vitendo kama vipo, itachukua hatua. Iwe kwa uwazi au kimya kimya,” anasema.

Mdau wa soka la wanawake kutoka Mkoa wa Shinyanga, Asia Jumanne anasema kwa sasa unyanyapaa umepungua tofauti na kipindi cha nyuma kwani watu wameanza kuelewa soka la wanawake kama biashara na ajira na jamii imeanza kusapoti.

Anasema wachezaji wa kike wameshindwa kuwa chapa kwa sababu ya kutumia majina ya wachezaji wengine, hasa wa kiume hali inayoleta tafsiri kuwa wanashindwa kujiamini na kulazimika kusimama kwenye kivuli cha jina la mchezaji wa kiume.

Mfano kuna wachezaji waliokuwa wakijiita majina ya kiume kama Shishimbi, Lunyamila, Mwalala na mengine mengi.

“Chapa ni muhimu hasa katika dunia ya sasa kwani kuna manufaa mengi mfano unaweza kuwa balozi, kuaminika na jamii inayokuzunguka ila changamoto mabinti zetu wanashindwa kujiamini kuwa chapa na kutumia majina ya wachezaji wengine hasa wa kiume hii inaweza kukupa tafsiri kuwa wanashindwa kujiamini,” anasema Asia.

Asia ambaye aliwahi kuwa Ofisa Habari wa Alliance Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake anasema kwa sasa kidogo kuna mabadiliko na kubadili mitazamo ya wachezaji wanawake, kwani awali ilionekana ukicheza mpira wa miguu lazima uishi maisha ya kiume wakati si kweli.

Kwa sasa angalau wameanza kubadilika na kubaki kwenye uhalisia wao na  kusema semina au mafunzo yanatakiwa kuongezeka ili kuwasaidia na hivyo kubadili mtazamo wa jamii katika kabumbu la wanawake.

Kuhusu chapa alisema wachezaji wengi hawana elimu kwa sababu wanaanza soka wakiwa wadogo wakiamini mpira utawatoa kimaisha na kutelekeza elimu, hivyo wanahitaji semina mbalimbali ili kuwasaidia kujitambua na waweze kujisimamia pia wazazi au walezi kuwalazimisha elimu ya darasani iende sambamba na kucheza soka ili iwasaidie katika maisha.

Kuhusu mapenzi ya jinsia moja, Asia anasema ni tatizo kwa dunia ya sasa na wachezaji wanaathiriwa na ulimbukeni wa teknolojia na ujana, hivyo watu wanaowasimamia wawawekee mazingira ya kuwaondoa katika tabia hiyo na kujiona wao ni wanawake na kuwatengenezea mazingira ya kutokaa (kulala) wawili wawili bali wakae zaidi ya wawili.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments