Tanesco kateni umeme kwa wote wanaodaiwa

 

ARUSHA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata umeme kwa wadaiwa wote wasiolipa gharama za kutumia umeme.

TANESCO inadai jumla ya Sh bilioni 224 kutoka Taasisi mbalimbali za serikali, binafsi na waliohama na madeni kutoka mita za zamani za umeme kwenda za kisasa, hali inayosababisha changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.

Amesema hayo leo, wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati alipokagua kituo cha umeme cha Lemuguru mkoani humo ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi  wa ujenzi  wa njia  kuu ya umeme  ya msongo wa KV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea Kenya (Kenya- Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP).-

“Hapa Arusha tu, TANESCO anadai wateja wake shilingi bilioni 7.7, na mara nyingi wanaodaiwa si wanachi wadogowadogo bali taasisi za serikali na wawekezaji wanaojiita wawekezaji wakubwa ambao ukiwakatia umeme wanakwambia unaua ajira.

“Wepesi wa kujificha kwenye kisingizio cha kulipa kodi na ajira. TANESCO anahitaji fedha ili awekeze na kisha awapelekee umeme wananchi, TANESCO nawaambia kateni umeme kwa mtu yeyote mnayemdai, ili mradi unamdai kwa haki, ” amesema Dk. Biteko.

Dk. Biteko pia ameagiza wadaiwa wote wa madeni ya bili za umeme wakalipe madeni hayo ili zipatikane fedha za kuwahudumia wananchi na ameongeza kuwa, serikali itaendelea kushughulikia changamoto za umeme nchini kwa aina mbalimbali ikiwemo kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme ukiwepo wa Julius Nyerere (MW 2115), ambao umefikia asilimia 94, ambapo amesema kuwa, mkandarasi ameshafunga mashine mbili tayari kwa kuanza majaribio ya kuzalisha umeme.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amekemea vikali wote wanaohujumu miundombinu ya umeme akitolea mfano wizi wa shaba na mafuta ambapo kati ya tarehe 25 Novemba, 2023 na 26 Novemba, 2024 kuna matukio 14 katika Ukanda wa Pwani ya kuharibu au kuhujumu miundombinu ya umeme, ambapo ameeleza kuwa, serikali itawashughulikia kwa kuendesha msako na watakapopatikana sheria itachukua mkondo wake.

Pia Dk. Biteko ameitaka TANESCO kuwasikiliza na kuwapatia majibu kwa haraka wananchi wanaopiga simu kwenye shirika hilo ili kupata huduma za umeme na mahali penye matatizo waambiwe.

“Huu utaratibu wa watu kupiga simu anaambiwa subiri, hii tumekubaliana kuwa haiwezekani ikaendelea na ndio maana nimewaambia kituo cha Huduma kwa Mteja tukiimarishe kutoka miito 65 na ziongezwe kufika 100 na zaidi,”  amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments