UEFA yaipa 5 Tanzania

 

 SHIRIKISHO la Mpira barani Ulaya (UEFA,) limeipongeza Tanzania kupitia Taasisi isiyo ya kiserikali ya Karibu Tanzania Organization (KTO,) kwa jitihada zinafanywa katika kukuza soka la wanawake na wasichana katika ngazi mbalimbali za Elimu kwa kuanzia ngazi ya Elimu Msingi.

Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na mtaalam wa michezo kutoka UEFA Carine Nkoue aliyetembelea shule za Uhuru, Kibugumo na Gezaulole zilizopo jijini Dar es Salaam.

Kupitia taasisi ya UEFA Foundation For Children ambao ni mahususi kwa kuendeleza soka kwa watoto na vijana ambapo Tanzania kupitia Program ya Mpira Fursa inayotolewa na KTO kupitia vyuo 54 vya maendeleo ya wananchi imekuwa mnufaika pekee wa Ukanda wa Afrika Mashariki.

Nkoue amesema, Tanzania inafanya kazi nzuri kupitia washirika wao wa KTO na amejionea namna mabinti wanavyojenga ujasiri kupitia soka la wanawake na wasichana.

“Mpira wa miguu sio kucheza pekee bali ni ajira, inajenga kujiamini kwa mabinti na kusaidia kujenga timu imara….kwa mchezo huu nilioshuhudia nina imani mabinti hawa watajenga timu imara zaidi katika level za juu….Tunategemea kuwaona katika soka la dunia,”amesema.

Aidha, amesema UEFA itaendelea kusimamia na kushiriki katika miradi ya namna hiyo kuhakikisha soka hususani kwa watoto wa kike linakuwa zaidi.

Pia amewapongeza walimu wa Shule za Msingi Kibugumo, Uhuru na Gezaulole kwa kujitoa na kuhakikisha wanafunzi wanashiriki katika soka pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa Pete na kriketi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa KTO Maggid Mjengwa amesema kupitia programu ya Mpira Fursa inayotolewa katika vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi imekuwa na matokeo chanya; kwa miaka minne ya utekelezaji wake umetoa wanawake wacheza soka, makocha wanawake pamoja na viongozi hali inayopelelea kukua kwa mpira wa miguu Tanzania.

Mjengwa amesema, ujio wa UEFA nchini ni kielelezo kuwa sekta ya michezo nchini ipo katika anga za kimataifa na hiyo ni kutokana na jitihada zinafanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya michezo kuanzia ngazi ya Elimu Msingi.

“Tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, TAMISEMI na Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF,) katika kusongesha gurudumu hili mbele zaidi,” amesema na kuongeza

” UEFA imeielewa na inaiamini Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya namna hii na sisi KTO tutaendelea kutafuta fursa zaidi kutoka UEFA ili sekta ya michezo iendelee kukua zaidi kimataifa.” amesema.

Amesema kuwa shule za Msingi 110 ambazo zipo karibu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) kote nchini zinanufaika na program ya Mpira Fursa ambayo pia imechangia katika kupunguza utoro kwa wanafunzi pamoja na kuwajengea mabinti kujiamini.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Wilaya ya Kigamboni Lucas Ouma ameishukuru UEFA kupitia mradi huo kwa watoto na kuahidi kuendelea kuhimiza programu ya michezo mashuleni kwa vitendo.

Amesema, wamekuwa wakishirikiana kwa ukaribu na Taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO,) katika kuhakikisha wanawajenga watoto kimichezo kuanzia ngazi ya chini kabisa.

Pia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gezaulole Mariam Kinande amesema, wamekuwa wakihamasisha wanafunzi kujiunga na michezo na takribani wanafunzi wa kike wapatao 64 wanashiriki mchezo wa Mpira wa miguu.

Katika ziara hiyo Nkoue ameshuhudia mechi ya kirafiki kwa timu za Wasichana wa Shule za Msingi Gezaulole ambayo iliibuka na ushindi wa mbao 2 -0 dhidi ya Kibugumo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments