Wanafunzi 100 kutofanya mtihani kidato cha 4

WANAFUNZI zaidi ya 100 wa shule huria ya Ukonga Skillful hawatafanya mtihani wa kidato cha nne utakaoanza Novemba 13, 2023 kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo utoro.

Hayo yamesemwa Diodorus Tabaro katika mahafali ya 17 ya shule hiyo iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam.

Amesema, changamoto kubwa ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo ni mdondoko wa wanafunzi ambao wamekuwa wakiacha shule kutokana na changamoto za kifamilia na tabia rika.

“Mdondoko wa wanafunzi unasababishwa na utoro, tabia rika, maisha magumu ya shule yanawakatisha tamaa, wengine wanakimbia kwa kuwa shule kuna sheria kali zinazowabana wakati wao wanataka kuwa huru”amesema.

Amesema, pia tatizo kubwa la shule huria hawana uwezo wa kuwabana mwanafunzi kuendelea kusoma na kwamba wamechukua maana ya huria kwenye maisha halisi.

“Kuna wanafunzi wanakuja kujisajili ndani ya mwezi mmoja haonekani, na wengine wanakuja kujisajili shule bila kuwataarifa wazazi au walezi na matokeo yake wanakosa wa kuwalipia ada wanaacha”amesema.

Tabaro pia ametoa lawama kwa wazazi ambao wamekuwa wakiishi na kuwalea watoto wao maisha ya kuigiza ‘Fake life’ ambayo uwaathiri watoto hata katika maisha yao ya kitaaluma.

“Wazazi wengi tumezaliwa maisha ya kawaida, lakinii ndani ya vichwa vya wazazi ni kutamani mtoto wake aishi maisha ya ‘standard’ ya juu, maisha ambayo hata kudeki mtoto hajui dada wa kazi ndio afanye, shuleni asifanye kazi, akitaka kitu fulani anapatiwa, mtoto anaweza kusema leo siendi kanisani, siendi msikitini mzazi anaona kawaida tu.

“Mtoto wa Sekondari anamiliki simu, anaingia mitandao ya Instagram, Facebook, TikTok, maisha ya huko kwenye mitandao sio maisha halisi, lakini wazazi ufurahi na kupenda na ujivunia kuona mtoto wake anatumia mitandao, tumesahau uhalisia.”amesema na kuongeza

“Lakini tunaposema ‘fake life’ hata shuguli ndogo za nyumbani hawezi, kumuachia familia kama wadogo zake kijana wa miaka 15 au 17 hawawezi kuwahudumia, maisha hayo yanawafuata mpaka kwenye maisha yao ya kitaalum;…. “mwanafunzi akipata kihoma kidogo tu unasikia naomba mpigie simu mami, mpigie dad, akimpigia analia na mzazi anaona ni jambo la kutisha, tunapaswa kuishi maisha ya uhalisia”alisisitiza Tabaro.

Naye Diwani wa Ukonga Ramadhani Bendera alihisii jamii kushirikiana na walimu katika malezi ili kujenga watoto wenye maadili mema.

Amesema Kata ya Ukonga imeunda kamati maalum ya kushughulika na changamoto za watoto wote wa Ukonga ikisimamiwa na Mtendaji wa Kata hiyo.

“Tabia rika sisi kama serikali tunapambana kuziondoa, tushirikiane tuziondoe kuanzia majumbani mwetu, kama serikali tutafanya kwa upande wetu, wazazi na jamii kwa ujumla nao watusaidie kwa upande wao, tutakuwa tunahudumia mashuleni na nyie wazazi muwahudumie majumbani. Mtoto alelewi na mzazi peke yake au mwalimu peke yake ni wa jamii nzima” amesema.

Awali, akisoma risala ya wanafunzi, mwanafunzi Debora Koroso alisema baadhi ya wazazi wanajisahau na hawafuatilii mienendo ya watoto wao na kujikuta wanajiingia kwenye tabia mbovu za uhuni, ulevi na kupelekea watoto kuanguka kitaaluma na wengine kuacha shule.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments