Wawili wakamatwa wakisafirisha dawa za kulevya

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 188 kwa makosa mbalimbali ikiwemo ya wizi na usafirishaji wa dawa za kulevya ambapo kati yao, wawili wamekamatwa na bunda 542 za madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni mirungi yenye uzito wa kilo 298.

Akitoa taarifa hiyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Salvas Makweli leo Novemba 14, 2023 amesema Jeshi hilo lilifanya operesheni maalumu kuanzia Oktoba 13, 2023 hadi Novemba 13, 2023 kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na matukio ya uhalifu na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

ACP Makweli amebainisha kuwa Novemba 12, 2023 muda wa saa 03:00 asubuhi huko katika maeneo ya Philips katika Halmashauri ya Jiji la Arusha walifanikiwa kumkamata Gilbert Joseph (33) mkazi wa Sinoni Jijini Arusha na Peter Waweru (33) mkazi wa nchi jirani wakiwa wanasafirisha madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni mirungi bunda 542 yenye uzito wa kilogramu 298, kwa kutumia gari aina ya Isuzu (namba zimehifadhiwa).

Aidha amesema watuhumiwa wote wawili wanaendelea kuhojiwa, pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.


Jeshi la Polisi mkoani humo linawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha limewataka watu wachache wanaojihusisha na uhalifu hususani madawa ya kulevya kuacha biashara hiyo ambayo inaharibu vijana wengi kwani wataendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments