WAZIRI MAVUNDE :NITAMALIZA MIGOGORO YA WACHIMBAJI WAKUBWA NA WADOGO

Facebo
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa uwepo wa taarifa sahihi za kijiolojia za miamba ndiyo zimebeba dhana ya utajiri na maisha bora kwa Watanzania.
Amesema hayo leo Novemba 10, 2023, jijini Dodoma, wakati akizungumza katika kipindi cha runinga na radio cha Good Morning kinachorushwa na Wasafi Media.

Amesema kuwa dhana ya Vision 2030, Madini ni Maisha na Utajiri ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini kwa kutengeneza matajiri wengi kupitia Sekta ya Madini sambamba na kuboresha maisha ya Watanzania na kwamba hayo ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona madini yanaleta maisha bora kwa Watanzania.
Waziri Mavunde amesema ili kutimiza malengo hayo, Serikali imekuja na mkakati wa kuiongezea uwezo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili ifanye utafiti wa kina wa miamba yote yenye madini iliyopo hapa nchini kwa lengo la kutengeneza kanzidata ya taarifa sahihi za kijiolojia.

“Malengo yetu ni kufanya tafiti za kina kwa angalau asilimia 50 kufikia asilimia 2030, ukilinganisha na sasa ambako ni asilimia 16 pekee ndiyo imefanyiwa utafiti wa kina kwa kutumia teknolojia ya kisasa, unaweza kuona mchango mkubwa iliyonao sekta ya madini pamoja udogo wa sehemu iliyofanyiwa utafiti wa kina wa miamba, sasa tukifanya mara tatu ya hapo tutakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi sambamba Pato la Taifa kwa ujumla” amesema Mhe. Mavunde

Aidha, amesema kuwa taarifa hizo zitaenda kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta zingine zikiwemo za Kilimo, Maji, Afya sambamba na uchumi kwa ujumla.

“Tukizungumzia maisha, tafiti hizi zitatuonesha sehemu maji yalipo, maji safi na salama ni muhimu kwa maisha ya watu wetu, lakini pia Wizara ya Kilimo ina mkakati wa kujenga mabwawa 100 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua zisizotabirika pia madini ya jasi yanasaidia kuondoa tindikali kwenye ardhi kwa ajili ya kilimo, mpaka hapo unaweza kuona jinsi sekta ya madini inavyogusa maisha wa Watanzania kupitia kilimo na maji.” amesema Mhe. Mavunde.

Amesema taarifa za tafiti hizo pia zitafungamanisha Sekta ya Afya kwa kuwa zitasaidia kujua miamba yenye gesi ya Hellium ambayo inatumika katika teknolojia ya upigaji picha za kina za anatomia (MRI), vipimo vinavyotumika hospitalini, na hivyo kuonesha jinsi sekta ya madini inavyoenda kugusa sekta ya afya.

Sambamba na hilo, Waziri Mavunde amesema kuwa uwepo wa taarifa hizo zitasaidia kuondoa migogoro baina ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwasababu chanzo cha migogoro hiyo ni wachimbaji wadogo kuamini madini yapo kwenye maeneo ya wachimbaji wakubwa kwa kuwa yamefanyiwa utafiti wa kina, hivyo migogoro hiyo itaisha baada ya kupata maeneo mengine yaliyofanyiwa tafiti.

“Tunataka Wachimbaji wadogo waache kuchimba kwa kubahatisha, madini sio ushirikina wala bahati ni sayansi, wachimbe kwa kuwa na uhakika kutokana na taarifa sahihi za kijiolojia, kwa kufanya hivi tutaokoa mitaji yao kwa kuwa watachimba kwa uhakika na kuuza madini wanayopata, watalipa mikopo waliyonayo, lakini pia watapata mikopo kwa kuwasilisha taarifa hizi kama dhamana katika taasisi za kifedha tofauti na sasa ambako wanalazimika kuweka dhamana nyumba, viwanja na mali zao zingine.” ameongeza Mhe. Mavunde.

Waziri Mavunde amehitimisha wiki ya Vision 2030, Madini ni Maisha na Utajiri ambapo Wizaya ya Madini na Taasisi zake zilipata fursa ya kuelezea mikakati na utekelezaji wa dira hiyo kufikia mwaka 2030.
*VISION 2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI*

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments