‘Wekeni programu kuboresha afya za wafanyakazi’

 

 CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), kimewaomba waajiri kuweka programu mbalimbali katika maeneo ya kazi zitakazosaidia kuboresha afya za wafanyakazi na kuleta tija sehemu za kazi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda alipoongoza ujumbe wa TUGHE kushiriki katika Coast City Marathon iliyofanyika mkoani Pwani, ambapo pamoja naye aliambatana na Mwenyekiti wa Kamati za Wanawake TUGHE Taifa, Catherine Katele pamoja na watumishi na wanachama wa TUGHE.

Mkunda ameeleza kuwa TUGHE inatambua umuhimu wa programu hizo katika sehemu kama za michezo pamoja na kufanya mazoezi ya mwili, kwani huimarisha afya za wafanyakazi na kuwakinga na hatari ya kupata magonjwa hasa yale yasiyo ya kuambukiza.

Pia amesema mazoezi huwaepusha na changamoto za afya ya akili, ambapo yasipodhibitiwa yanaweza kuleta athari kubwa ikiwemo kushuka kwa uzalishaji katika maeneo ya kazi.

Mkunda amewataka wafanyakazi kushirikiana kikamilifu na vyama vya wafanyakazi katika maeneo ya kazi, ikiwewamo kujiunga na vyama hivyo, ili kuleta umoja miongoni mwao na pia kuboresha afya zao.

Mgeni rasmi katika Marathoni hiyo iliyolenga kuchangia ujenzi wa wodi ya wazazi katika Hospital ya Rufaa ya Tumbi, alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge aliyemwakilisha Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambaye amewaomba wadau kuendelea kushirikiana na serikali kuunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya afya nchini.

TUGHE imekuwa ikishirikiana mara kwa mara na wadau mbalimbali kuboresha sekta ya afya nchini, ikiwemo kutoa misaada ya vifaa katika hospitali kwa kuzingatia kuwa wanachama wa TUGHE pia wanatoka katika sekta hiyo ya afya pamoja na serikali.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments