kilele cha Tamasha la Kumbukumbu ya mzalendo wa Kiafrika, mpigania Uhuru na muasisi wa Umoja wa Wanawake Tanzania ( U.W.T), Bibi Titi Mohamed Salum, tuna kila sababu ya kujivunia mwanamke shupavu.
Bibi Titi Mohamed ni Mwanamajumui wa Kiafrika aliyejitoa kupigania Uhuru sio tu wa Tanganyika, bali katika upwa wa Afrika Mashariki. Akiwa kijana mbichi kabisa Bibi Titi ametumia muda wake mwingi kuitangaza TANU na kupigania Uhuru wa Tanganyika.
Ni Bibi Titi aliyeanza kupaza sauti ya haki za wanawake katika mikutano ya TANU na hasa mkutano wake wa mwanzo uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam alipotaka kuondolewa kwa pazia la uzio wa kuwatenga mbali wanawake katika mikutano ya hadhara.
Moto wa Bibi Titi ulisambaa kuanzia viunga vya Mzizima ambayo ni Dar es Salaam ya sasa hadi Unyenyembe, Tabora, aliwakusanya wanawake akiwaeleza haki zao, nguvu zao katika siasa na mengineyo.
Unapoiona U.W.T ya leo yenye mafanikio basi fahamu kuwa kuna jasho jingi la Bibi Titi Mohamed limetiririka, nguvu na muda wake akijitolea hali na mali kuisimamisha Jumuiya hiyo akitetea maslahi na haki za wanawake na jamii nzima kwa ujumla.
Kadi yake ya uanachama wa TANU ilikuwa namba 16. Wengi wa wanawake waliofuatwa kuongoza Tawi la Wanawake wa TANU karibu wote walimtaja Bibi Titi kuwa ni hodari, shupavu na ndie anaeweza kuongoza Tawi la Wanawake ndani ya TANU.
Leo ni siku muhimu sana katika historia ya nchi yetu na katika hili, tunakila sababu ya kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa, ambaye atabaki katika kumbukumbu kwa kuanzisha jambo muhimu la kumuenzi muasisi wa Taifa letu, Mwanamajumui wa Kiafrika, Bibi Titi Mohamed.
Pengine kama si jitihada na msimamo wake Mchengerwa kuhusu kumuenzi Bibi Titi Mohamed, leo hii kusingekuwa na lolote la kukumbukwa zaidi ya barabara mojawapo jijini Dar es Salaam iliyopewa jina la mpigania Uhuru huyo Bibi Titi.
Nampongeza Mbunge wa Rufiji kwa kumuenzi kwa vitendo Mpigania Uhuru na Mwanamajumui wa Kiafrika, Bibi Titi Mohamed.
*Mwandishi wa makala haya amepata kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zanzibar.
0 Comments