ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeanza ujenzi wa maduka ya kisasa darajani Bazaar, eneo la kuegeshea magari la kisasa, pamoja na vituo vya kisasa vya mabasi.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo leo Desemba 21 ,2023 alipoweka jiwe la msingi mradi wa maegesho ya magari Malindi kuelekea shamrashamra za miaka 60 ya Mapinduzi Viwanja vya Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha,Amesema lengo la Serikali ni kuwa na mji wa kisasa utakaotoa huduma zote kwa wananchi ikiwemo usafiri wa umma wa mabasi na vituo vyake, maegesho ya magari ya kisasa pamoja na biashara.
Pia, Rais Mwinyi ameeleza kuwa yanayofanyika ni kwa nia njema kulinda urithi wa dunia kwa maeneo yote ya Mji Mkongwe kwa kuzingatia masharti na taratibu za Shirika la Umoja wa Mataifa UNESCO kwa utekelezaji wa miradi maendeleo nchini.
Kwa upande mwingine, Dk Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kujenga miradi mikubwa ya maendeleo na kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025.
Mradi huo wa kisasa wa maegesho ya magari unajengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6 na magari zaidi ya 200 yataegeshwa kwa wakati mmoja.
0 Comments