Majaliwa ateta na Balozi wa Saudi Arabia

 WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Yahya Ahmed Okeish na kujadiliana masuala mbalimbali yakiwemo ya kilimo, uvuvi na uwekezaji.

Akizungumza na balozi huyo leo Desemba 13, 2023 ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema anatambua matunda ya uhusiano wa muda mrefu ambayo Tanzania imeyapata  kutoka Saudi Arabia ikiwemo misaada kwenye sekta za afya, elimu na maji.

“Natambua dhamira ya Saudi Arabia kuja kuwekeza kwenye kilimo, wakiwa tayari tutawapokea na natumaini watatumia vizuri fursa hiyo kuendeleza kilimo. Lakini pia tunazo fursa za uwekezaji za uvuvi kwa Tanzania Bara na Zanzibar” amesema kiongozi huyo.

Aidha,Waziri Mkuu ameishukuru nchi hiyo kwa kukubali kununua nyama kutoka Tanzania na akatumia fursa hiyo kuwaomba waongeze wigo wa kununua nyama zaidi na kuwahakikishia kwamba Tanzania itaendelea kuwapatia nyama yenye viwango bora.

Pia,ameipongeza serikali ya nchi hiyo kwa uamuzi wake wa kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kumpongeza Mfalme wa nchi hiyo, King Salman Bin Abdulaziz Al Saud na Waziri Mkuu wake, Mwanamfalme Mohammed Bin Salman Bin Abdulaziz Al Saud kwa ushindi ambao nchi yao imeupata ili kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa Duniani ya Expo 2030.

Maonesho hayo makubwa duniani, yanatarajiwa kufanyika jijini Riyadh kuanzia Oktoba, 2030 hadi Machi 2031.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments