“Marufuku kununua madini hotelini”

NAIBU Waziri wa Madini,Dk Steven Kiruswa amepiga marufuku wageni kutoka nje ya nchi kununuwa madini wakiwa hotelini kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua ikiwa nia pamoja na kukamatwa na kushtakiwa.

Dk Kiruswa alisema hayo katika kijiji cha Mundarara chenye sifa ya uchimbaji madini ya Ruby kilichopo katika wilaya ya Longido Mkoani Arusha wakati akiongea na wawekezaji wa madini hayo,viongozi wa vijiji vyote vya kata ya Mundarara na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Longido.

Alisema ni kosa kisheria mgeni kufanya biashara akiwa hotelini kwani serikali lazima itakuwa inakosa mapato kwani hakuna uhakika rasmi wa biashara hiyo  inayofanyika huko kwa kificho na kanuni na sheria za madini haziruhusu mgeni kufanya biashara ya madini bila ya kuwa na mbia mzawa.

Waziri aliwataka wafanyabiashara wa madini ya Ruby na madini mengine nchini kuacha mara moja tabia hiyo ya kuhifadhi wageni hotelini na kufanya biashara haramu ya kununua madini kwa kijicho kwani dola haitawacha salama.

Alisema serikali imejenga mazingira mazuri ya kufanya biashara ya madini kwa wawekezaji,wachimbaji wakubwa na kati na wachimbaji wadogo lakini inasikitisha kuona bado watu hawaridhiki na mazingira hayo sasa serikali haitakuwa na huruma kwa wale wenye nia ovu yenye lengo la kujitajilisha na kuvunja sheria.

Dk Kiruswa alisema serikali iko macho na inajua kila kitu na wakati ukifika wale wote wenye kufanya biashara haramu ya madini dola itawakamata kwani hawana nia njema na serikali.

‘’Ukikutwa umemhifadhi mgeni hotelini na unashirikiana naye kufanya biashara ya kununuwa madini na kwenda kuuza nje bila kufuata sheria serikali haitakuacha salama lazima ushughulikiwe kisheria kwani wewe ni muhujumu uchumi’’ alisema Kiruswa

Akizungumzia utoroshaji wa madini nje ya nchi kwa njia ya panya,Waziri Kiruswa aliwataka wawekezaji wa madini ya Ruby na madini mengine kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kukiuka taratibu na watashikwa kwani dola iko kila mahali na inafuatilia nyendo zote kwa ukaribu.

Dk Kiruswa alisema serikali inajitahidi kila kukicha kujenga mazingira mazuri ya wachimbaji madini na wafanyabiashara wa sekta hiyo lakini kuna baadhi yao hawana nia njema kazi kupanga mikakati haramu ya kufanya biashara haramu ikiwa ni pamoja na kutorosha madini bila kufuata taratibu.

Alisema kwa sasa hilo halitavumiliwa na kuwatahadharisha wafanyabiashara wa madini kote nchini kuacha mara moja tabia ya kutorosha madini nje kunainyima serikali kuongeza mapato katika sekta hiyo.

Aidha Waziri Kiruswa aliwashukuru viongozi wa bodi ya Mgodi wa Ruby unaomilikiwa na kijiji cha Mundarara kwa kumaliza mgogoro na mwekezaji mzawa Rahimu Mollel maarufu kwa jina la Pendeza kwa kukaa pamoja na kuondoa tofauti zilizokuwa zikijitokeza na kwa kufanya hivyo kunaweza kuleta maendeleo katika kijiji hicho kwa maslahi ya wanachini wote.

Waziri pamoja hilo alimtaka Afisa madini Mkoa wa Arusha(RMO) kushughulikia changamoto za wachimbaji madini ya Ruby kwa wakati ili kujenga imani kwa wachimbaji na serikali yao kuliko kukaa muda mrefu bila kutatua changamoto zinazowakabili kwani kunaweza kuleta sitafamu ambayo haina msingi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments